Jun 14, 2024 06:50 UTC
  • Jibu erevu la Hamas kwa mpango wa Biden na kutupwa mpira kwenye uwanja wa Netanyahu

Ismail Haniyeh, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas, na Ziad al-Nakhaleh, katibu mkuu wa harakati ya Jihad Islami, wameongoza makundi mawili hayo ya mapambano ya ukombozi wa Palestina, katika kujibu mpango wa kusitisha mapigano na kubadilishana mateka katika kikao na Waziri Mkuu wa Qatar na vile vile wakatuma jibu hilo kwa viongozi wa Misri.

Katika jibu hilo la makundi ya muqawama, maslahi ya wananchi wa Palestina, ulazima wa kusitishwa kabisa vita na kuondoka kikamilifu vikosi vya wavamizi katika Ukanda wa Gaza vimepewa kipaumbele.

John Kirby, msemaji wa Baraza la Usalama la Kitaifa la White House, amesema kuwa Marekani imepokea majibu ya Hamas kupitia wapatanishi na kuwa inachunguza kwa makini majibu yake.

Katika mkutano na waandishi wa habari akiwa na mwenzake wa Qatar mjini Doha, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Anthony Blinken, wakati akithibitisha kupokea majibu ya Hamas, alifafanua kuwa Hamas imetaka kufanyike marekebisho katika mpango huo, jambo ambalo amesema linakubalika.

Hata hivyo gazeti la Kizayuni la "Yediot Aharnot" linalochapishwa katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) Jumanne usiku lilimnukuu afisa mmoja wa Kizayuni na kudai kuwa, harakati ya Hamas ilikataa mapendekezo ya Rais Joe Biden wa Marekani kuhusiana na kufanyika marekebisho hayo.

Katika taarifa yake, harakati ya Hamas imesisitiza kuwa siku zote imekuwa ikitoa wito wa kusitishwa vita na kubadilishana mateka na wakati huohuo kukaribisha wazi mpango wa Joe Biden na azimio la Baraza la Usalama, lakini ni utawala ghasibu wa Israel ndio umekuwa ukipinga jambo hilo.

Majibu ya Hamas yametolewa baada ya azimio lililopendekezwa na Marekani kuhusu usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza kupitishwa bila upinzani au kura ya turufu katika kikao cha baraza hilo siku ya Jumatatu.

Azimio hilo limepitishwa katika hali ambayo katika kipindi cha miezi minane iliyopita, Marekani, imekuwa ikizuia kupitishwa azimio lolote la kusitisha mapigano huko Gaza na kuilaani Hamas kutokana na operesheni yake ya kijeshi ya Kimbunga cha al-Aqsa mnamo Oktoba 7, mwaka jana na kushirikiana kwa karibu na Israeli ili kuikandamiza harakati hiyo ya kupigania ukombozi wa Plaestina.

Ziad Nakhaleh (kushoto) na Ismail Haniyeh

Azimio nambari 2735 la Baraza la Usalama, ambalo lina vifungu saba, linasema kuwa azimio lililopendekezwa na Marekani linakumbusha maazimio yote muhimu kuhusu hali ya Mashariki ya Kati, likiwemo suala la Palestina, na kutambua juhudi za kidiplomasia zinazofanywa na Misri, Qatar na Marekani kwa lengo la kufikia mkataba wa kusitisha mapigano utakaotekelezwa katika hatua tatu.

Awamu ya kwanza itahusisha kusitishwa mapigano mara moja, kuachiliwa mateka wakiwemo wanawake, wazee na majeruhi, kurejeshwa miili ya baadhi ya mateka waliokufa, kubadilishana wafungwa wa Kipalestina, kuondolewa Wazayuni kwenye maeneo yenye watu wengi huko Gaza, kurejea raia wa Palestina katika makazi na vitongoji vyao katika maeneo yote ya Gaza, ikiwa ni pamoja na kaskazini na vile vile kuwezeshwa usambazaji salama na wa kiwango kikubwa wa misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.

Awamu ya pili itajumuisha makubaliano ya pande zote kwa ajili ya kumaliza kabisa uhasama, mkabala wa kuachiliwa mateka wote ambao watakuwa bado wako Gaza na kuondoka kabisa vikosi vya Israeli katika ukanda huo.

Hatua ya tatu itahusiana na kuanzishwa mpango mkubwa wa ukarabati na ujenzi mpya wa Gaza ambao utachukua miaka kadhaa na kurejeshwa kwa familia zao miili ya mateka wote waliouawa ambao bado wako Gaza.

Azimio hilo linasisitiza kuwa iwapo mazungumzo ya awamu ya kwanza yatadumu kwa zaidi ya wiki sita, usitishaji vita utaendelea maadamu mazungumzo yatakuwa yanaendelea, na kuwa Marekani, Misri na Qatar zinapasa kuhakikisha kuwa mazungumzo hayo yanaendelea hadi makubaliano yote yatakapokamilika.

Majibu ya Hamas kwa pendekezo la Joe Biden sio tu kukubali au kukataa mapendekezo yaliyowasilishwa, bali yanajumuisha mambo mengi, ikiwa ni pamoja na usitishaji wa kudumu wa mapigano, kuondolewa kabisa vikosi vya uvamizi kutoka Gaza, kuanza ujenzi mpya katika Ukanda wa Gaza, kurejea wakimbizi kwenye maeneo yao, kubadilishana mateka na mambo mengine yaliyojadiliwa katika mpango wa kusitisha mapigano.

Sasa, kwa kutangazwa msimamo wa vikosi vya muqawama na Hamas, mpira sasa uko kwenye uwanja wa Israeli na Marekani, ambazo lazima zifuate kile zimekuwa zikikisisitiza mara nyingi ili kufikia makubaliano ya usitishaji vita wa kudumu na kuondolewa vikosi vya uvamizi katika Ukanda wa Gaza. Kwa hakika, kwa kuukubali mpango uliopendekezwa wa Biden, Hamas sio tu imethibitisha dhamira yake ya kusimamisha vita na kuwaondolea watu wa Gaza mashinikizo yaliyowekwa, bali pia imepelekea kudhihiri wazi zaidi upinzani wa nyuma ya pazia wa Israel na baraza la mawaziri la mrengo wa kulia la Netanyahu dhidi ya mpango huo wa Netanyahu na hivyo kuongeza uwezekano wa kuibuka tena tofauti kati ya Biden na Netanyahu. Ni wazi kuwa suala hilo linaweza kuongeza pengo la hitilafu ndani ya baraza la mawaziri la Netanyahu, na hatimaye kulipelekea kusambaratika.