Jun 19, 2024 11:16 UTC
  • Hizbullah yashambulia kiwanda na kambi za kijeshi za Israel

Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imeshambulia kwa makombora na ndege zisizo na rubani kiwanda na kambi kadhaa za kijeshi za utawala wa Kizayuni Israel huko kaskazini mwa ardhi za Palestina zilizopachikwa jina bandia la Israel, kujibu chokochoko za jeshi hilo katili.

Televisheni ya al-Manar ya Lebanon imenukuu taarifa ya Hizbullah inayosema kuwa, wanamapambano wa harakati hiyo ya muqawama mapema leo Jumatano, wameshambulia kwa makombora na droni mikusanyiko ya wanajeshi na timu za lojistiki za Wazayuni katika mji wa Metula.

Taarifa ya Hizbullah imeongeza kuwa, makombora na droni hizo zimelenga shabaha zilizokusudiwa kwenye operesheni hiyo ya ulipizaji kisasi, na kulisababishia jeshi la Kizayuni hasara kubwa.

Harakati ya Hizbullah imesema imefanya operesheni hiyo kulipiza kisasi, baada ya Wazayuni maghasibu kushambulia kwa droni gari lililokuwa limebeba mkimbizi wa Kipalestina katika mji wa Borgholiya, kusini mwa Lebanon. Imemtaja mkimbizi huyo kama Mohammed Yousef al-Hassan, na kueleza kuwa alikuwa akiishi katika kambi ya Qasimia karibu na wilaya ya Tyre.

Aidha juzi Jumatatu, kamanda mwingine mwandamizi wa Hizbullah, Muhammad Mustafa Ayoub aliuawa shahidi katika shambulio la ndege isiyo na rubani (droni) ya utawala katili wa Israel viungani mwa mji wa Salaa katika wilaya ya Tyre.

Utawala wa Israel umekuwa ukishambulia mara kwa mara eneo la kusini mwa Lebanon tangu tarehe 7 Oktoba mwaka uliopita, ulipoanzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Aidha Hizbullah imekuwa ikifanya mashambulizi ya maroketi karibu kila siku dhidi ya maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu (Israel), ili kuonyesha mshikamano wao na Wapalestina wasion na ulinzi wa Gaza.

Tags