Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina atembelea Rwanda
Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, leo Jumamosi ameelekea mjini Kigali Rwanda kwa ajili ya kushiriki mkutano wa nchi za Umoja wa Afrika AU.
Majdi al Khalidi, mshauri wa Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amenukuliwa na mtandao wa habari wa al Yaumus Sabi'i akisema kuwa, mbali na kutembelea Rwanda, Mahmoud Abbas atatembelea pia nchi nyingine moja ya Afrika na moja ya barani Ulaya.
Amesema, akitoka Rwanda, Mahmoud Abbas ataelekea nchini Sudan na baadaye nchini Ufaransa ambako anatarajiwa kukutana na Rais François Hollande wa nchi hiyo pamoja na John Kerry, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani.
Mkutano wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika AU unatarajiwa kuanza kesho huko Kigali, mji mkuu wa Rwanda.