Wapalestina washiriki mkutano wa ustawi wa biashara wa mjini Nairobi
Duru za Palestina zimetangaza kuwa, ujumbe wa kiuchumi wa Wapalestina unashiriki katika Mkutano wa 14 wa Biashara na Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNCTAD) unaofanyika mjini Nairobi Kenya.
Shirika la habari la Qudsuna limeripoti habari hiyo leo na kusema, ujumbe wa kiuchumi wa Palestina unaoongozwa na Bi Abeer Odeh, Waziri wa Uchumi wa Palestina, unashiriki katika mkutano huo ulioanza leo Jumapili jijini Nairobi.
Mkutano wa siku sita wa Biashara na Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNCTAD) utaendelea hadi tarehe 22 mwezi huu wa Julai.
Ikumbukwe kuwa mwezi Novemba 2012, Palestina iliimarisha uachama wake ndani ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kutoka taasisi muangaliaji na kuwa serikali muangaliaji ndani ya umoja huo.
Kuongezeka itibari ya Palestina ndani ya Umoja wa Mataifa kumelipa fursa taifa hilo ya kuomba uanachama katika mashirika mbalimbali ya umoja huo na kuwa na nafasi kubwa zaidi katika masuala mbalimbali ya kimataifa.