Pakistan yakanusha ripoti za Israel kuhusu kuipatia Iran silaha za nyuklia
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistani, Mumtaz Zahra Baloch, amekanusha ripoti zilizochapishwa na vyombo vya habari vya Israel zinazodai kuwa Islamabad imejitolea kupeleka silaha za nyuklia nchini Iran, na kuzitaja ripoti hizo kuwa hazina msingi wowote.
Zahra Baloch amesema katika mkutano wake na waandishi wa habari wa kila wiki kwamba: "Ripoti kama hizo ni za uongo, na kabla ya kuzitilia maanani, ni muhimu kufikiria juu ya chanzo cha chake, msingi na ajenda mbovu iliyo nyuma yake."
Gazeti la Israel la Jerusalem Post limedai kuwa Pakistan inakusudia kuipatia Iran makombora ya masafa ya kati ya Shaheen-3, yenye uwezo wa kubeba vichwa vya nyuklia.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan amekadhibisha madai hayo na kulaani vita vya Israel katika Ukanda wa Gaza. Mumtaz Zahra Baloch pia ametoa wito wa kusitishwa mapigano na kuboresha mchakato wa kuwasilisha misaada ya kibinadamu kwa watu wanaoendelea kuuawa wa Ukanda wa Gaza.
Israel imeendelea kupuuza azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kusimamisha vita mara moja, na amri ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki iliyoutaka utawala huo ghasibu kuchukua hatua za kuzuia vitendo vya mauaji ya kimbari na kuboresha hali mbaya ya kibinadamu huko Gaza.