Aug 10, 2024 11:13 UTC
  • Muqawama: US ni mshiriki wa mauaji mapya ya halaiki Gaza

Makundi ya mrengo wa Muqawama katika eneo la Asia Magharibi yamelaani vikali jinai mpya ya kuogofya ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza, ambapo zaidi ya Wapalestina 100 wameuawa shahidi na makumi ya wengine kujeruhiwa.

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imesema katika taarifa kuwa: Mauaji ya halaiki katika shule ya al-Tabieen katika kitongoji cha al-Daraj katikati mwa mji wa Gaza ni uhalifu wa kutisha ambao unaashiria kuongezeka kwa uhalifu na mauaji makubwa katika historia ya vita, vilivyofanywa na Wanazi wapya katika Ukanda wa Gaza.” 

Imeeleza kuwa, Harakati ya HAMAS tunathibitisha kwamba kuongezeka kwa jinai za Wazayuni na ukiukwaji mkubwa dhidi ya raia wasio na ulinzi katika maeneo yote ya Ukanda wa Gaza hakungeendelea bila ya uungaji mkono wa moja kwa moja wa Marekani, jambo ambalo linaifanya Marekani kuwa mshiriki kamili katika jinai hizi."

Aidha Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina imesema kuwa, shambulio hilo la mabomu dhidi ya shule ya "al-Tabieen" katika kitongoji cha Al-Daraj ni "uhalifu kamili wa kivita." Imebainisha kuwa, "Visingizio vya jeshi la adui kwa kuharibu shule ni vile vile vilivyotumika kuharibu hospitali hapo awali, na vimethibitishwa kuwa vya uwongo."

Wakati huo huo, Harakati ya Ansarullah ya Yemen imesema, "Maadui wamefanya mauaji ya kikatili, kwa usaidizi kamili wa Marekani, dhidi ya watu waliokimbia makazi yao wakati walipokuwa wakiswali Swala ya Alfajiri ndani ya shule katikati ya jiji la Gaza."

Jinai ya kuogofya ya Israel kwa ushirikiano na US huko Gaza

Msemaji wa Ansarullah, Mohammed Abdul-Salam amesema katika taarifa kuwa, "Tunalaani vikali ufashisti wa Kizayuni, na tunalaani uungaji mkono kamili wa Marekani kwa Israel ambayo inaendelea kufanya uhalifu wa mauaji ya halaiki huko Gaza."

Alfajiri ya leo, utawala khabithi wa Israel umeshambulia kwa mabomu shule ya "Al-Tabieen" katika kitongoji cha Al-Daraj baada ya Swala ya Alfajiri na kuua shahidi Wapalestina zaidi ya 100, huku duru zikiarifu kwamba, idadi ya waliouawa inaweza kuongezeka kutokana na kuwepo kati ya watu 4,000 hadi 5,000 katika shule hiyo. Ukumbi wa Swala ulikuwa na watu 250 wakati wa shambulio hilo la kinyama.

Tags