Al Azhar yalaani jinai mpya za Wazayuni; Tunisia wamuunga mkono Sinwar
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i115076-al_azhar_yalaani_jinai_mpya_za_wazayuni_tunisia_wamuunga_mkono_sinwar
Chuo Kikuu cha Kiislamu cha al Azhar cha Misri kimelaani vikali jinai mpya ya utawala wa Kizayuni ya kuwaua kikatili Waislamu waliokuwa wanasali katika kambi ya wakimibizi huko Ghaza na kusisitiza kuwa, maneno ya kuelezea jinai na ukatili mbaya mno wa Wazayuni, hayapatikani.
(last modified 2024-08-11T00:53:25+00:00 )
Aug 11, 2024 00:53 UTC
  • Al Azhar yalaani jinai mpya za Wazayuni; Tunisia wamuunga mkono Sinwar

Chuo Kikuu cha Kiislamu cha al Azhar cha Misri kimelaani vikali jinai mpya ya utawala wa Kizayuni ya kuwaua kikatili Waislamu waliokuwa wanasali katika kambi ya wakimibizi huko Ghaza na kusisitiza kuwa, maneno ya kuelezea jinai na ukatili mbaya mno wa Wazayuni, hayapatikani.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, Chuo Kikuu cha Al Azhar cha Misri jana Jumamosi kilitoa taarifa ya kulaani jinai hizo za kutisha za Israel katika kambi ya wakimbiizi ya al Daraj katika Ukanda wa Ghaza na kusisitiza kuwa, ukatili huo ni mkubwa kupindukia kiasi kwamba hakuna maneno ya kuweza kuuelezea. 

Katika upande mwingine, Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imetoa taarifa ya kulaani jinai hiyo ya Israel na kusema kuwa, ukatili huo wa utawala wa Kizayuni umefanyika wakati huu ambapo mazungumzo ya kusimamisha vita yanaendelea na hii ni kuthibitisha kuwa utawala huo dhalimu hauna nia kabisa ya kukomesha jinai zake huko Ghaza.

Chuo Kikuu cha al Azhar cha Misri

Hii si mara ya kwanza wala ya pili na wala ya mwisho ya utawala wa Kizayuni kufanya jinai za kutisha dhidi ya Wapalestina wasio na ulinzi. Baya zaidi ni kwamba jinai hii ya jana Jumamosi imefanywa na Israel dhidi ya Waislamu waliokuwa katikati ya Sala ya Alfajiri bila ya silaha bali kwenye mazingira ya kiraia kikamilifu.

Katika upande mwingine, wananchi wa Tunisia wamefanya maandamano ya kulaani jinai za Israel na wamemuunga mkono Yahya Sinwar, Mkuu mpya wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS. Maandamano ya wananchi wa Tunisia yameitishwa na asasi za kiraia ambapo sambamba na kulaani jinai za kutisha za Israel, waandamanaji wametangaza uungaji mkono wao wa pande zote kwa Yahya Sinwar, mkuu mpya wa masuala ya kisiasa wa HAMAS.