Aug 14, 2024 04:06 UTC
  • Putin: Russia inafanya kila kitu kuunga mkono Palestina

Rais Vladmir Putin wa Russia ameeleza machungu na wasiwasi mkubwa kuhusu maafa wanayopata raia Wapalestina katika Ukanda wa Gaza kutokana na mauaji ya kimbari yanayotekelezwa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika eneo hilo.

Putin ameyasema hayo mjini Moscwo wakati akimpokea Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina Mahmoud Abbas kwa lengo kujadili hali ya Asia Magharibi kwa kuzingatia uhasama wa Israel dhidi ya watu wa Palestina.

Taarifa ya Kremlin imesema, Putin alimpokea Abbas katika Ikulu ya Kremlin siku ya Jumanne, ambapo viongozi hao wawili walibadilishana mawazo juu ya hali ya Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) kwa kuzingatia hali ya sasa ya 'mzozo wa Israel na Palestina' na maafa makubwa ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.

Putin alimwambia kiongozi wa Palestina kwamba Moscow "inafanya kila kitu ... kusaidia Palestina na watu wa Palestina."

Mahmoud Abbas, kwa upande wake, alipongeza juhudi za Moscow za kufanikisha maridhiano ya Wapalestina na kuitaja Russia kuwa "moja ya marafiki wapendwa wa watu wa Palestina."

Kiongozi wa Urusi siku zote amekuwa muungaji mkono mkubwa wa watu wa Palestina na kuanzishwa kwa taifa huru la Palestina.

Putin alisema njia pekee ya kuleta "amani ya kudumu, ya kutegemewa na tulivu katika eneo hilo," ni utekelezaji wa maazimio yote ya Umoja wa Mataifa na "kuundwa kwa taifa lenye mamlaka kamili la Palestina."

Abbas alisema alisafiri kwenda Moscow "ili kubadilishana mawazo na Putin kuhusu hali ngumu ambayo Palestina inapitia, na kujadili njia za kukomesha uchokozi na vita vya maangamizi vinavyoendeshwa na utawala wa Israel huko Gaza na Ukingo wa Magharibi."