Aug 19, 2024 03:08 UTC
  •  Kiwewe cha shambulizi la kilipiza kisasi la Iran; Safari zote za ndege za Marekani kwenda Israel zafutwa

Shirika la Redio na Televisheni la Israel limetangaza kuwa safari zote za ndege za Marekani kuelekea katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel) zimefutwa.

Uamuzi huu umechukuliwa kutokana na woga na hofu ya mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran dhidi ya mauaji ya kigaidi yaliyofanywa na Israel dhidi ya aliyekuwa mkuu wa Idara ya Siasa ya harakati ya Hamas, Ismail Hamiyeh, akiwa ugenini mjini Tehran, mwezi uliopita. 

Shirika la Redio na Televisheni la Israel limetangaza kuwa mashirika ya ndege ya Marekani yamefuta rasmi safari zote za ndege "kwenda na kutoka" Israel hadi Aprili 2025.

Hapo awali, gazeti la Israel la "Israel Hayom" liliandika kwamba kampuni kuu ya ndege ya "American Airlines" imefuta safari zake za kwenda Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel) hadi Aprili 2025.

Ripoti ya gazeti hilo imesema, kwa sasa hakuna ndege za moja kwa moja kwenda na kutoka Israel msimu ujao wa baridi kwenye tovuti ya American Airlines.

Kabla ya hapo, Shirika la Ndege la Delta lilitangaza kuwa limefuta safari zake za ndege kutoka New York hadi Tel Aviv hadi Agosti 31 mwaka huu.

Mashirika ya ndege ya Bulgaria, Lithuania na Ethiopia pia yametangaza kusitisha safari zao za kuelekea Israel.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu

Wasiwasi na mkanganyiko wa kinafsi wa Wazayuni kutokana na jibu lisiloepukika la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na kuuawa kigaidi Ismail Haniyeh, mkuu wa Idara ya Siasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) na majibu ya Hizbullah ya Lebanon dhidi ya mauaji ya shahidi Fawad Shukr, mmoja wa makamanda wake wakuu, vimezidisha matatizo ya kinafsi na kisaikolojia ya Wazayuni ambao wanaendelea kufanya mauaji ya kimbari huko Palestina kwa zaidi ya miezi 10 sasa.

Vyombo vya habari vya Israel pia vimekiri kwamba, baada ya kuuawa shahidi Haniyeh, Wazayuni wanasubiri kwa hofu kubwa majibu ya Iran kwa mauaji hayo.

Tags