Aug 30, 2024 02:40 UTC
  • Umoja wa Ulaya kuwawekea vikwazo mawaziri wa Israel

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell amewataka mawaziri wa mambo ya nje wa EU kuzingatia vikwazo dhidi ya mawaziri wa Israel.

Borrell jana ya Alkhamisi aliwaambia waandishi wa habari kwamba, atawaasa mawaziri wa mambo ya nje wa umoja huo kuzingatia vikwazo dhidi ya mawaziri wa Israel, ambao wamekuwa wakitoa na kusambaza "jumbe za chuki zisizokubalika dhidi ya Wapalestina."

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Umoja wa Ulaya amezitaka nchi wanachama wa EU kuwawekea vikwazo baadhi ya mawaziri wa Israel ambao wamekuwa "wakipendekeza mambo ambayo yanaenda kinyume na sheria za kimataifa" akisisitiza kuwa kitendo hicho ni kuchochea moto wa "kufanya uhalifu wa kivita."

Mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa kwa mwezi wa 11 sasa huko Ghaza, ambayo yamepelekea kuuawa shahidi zaidi ya watu 40,000 na kujeruhiwa wengine zaidi ya 95,000, hayajashuhudia uchukuaji hatua madhubuti na za maana wa jamii ya kimataifa hususan Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya.

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell

Mashambulizi na vikwazo dhidi ya Ukanda wa Gaza vimesababisha uhaba mkubwa wa chakula, maji safi na dawa, na kuacha sehemu kubwa ya eneo hilo lililozingirwa kuwa magofu.

Israel inakabiliwa na tuhuma za mauaji ya halaiki katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ambayo imeamuru kusitishwa kwa operesheni za kijeshi katika mji wa kusini wa Rafah, ambapo zaidi ya Wapalestina milioni moja walikuwa wametafuta hifadhi kabla ya eneo hilo kuvamiwa Mei 6.

 

Tags