Sep 09, 2024 06:50 UTC
  • US yaja na mpango mpya wa kusitisha vita Ghaza,

Maafisa wa Marekani na wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamesema, Washington "haina matumaini" ya kufikiwa makubaliano ya kubadilishana mateka na makundi ya Palestina katika Ukanda wa Ghaza, lakini pamoja na hayo, karibuni hivi itawasilisha pendekezo lake jipya.

Shirika la utangazaji la Israel KAN limewanukuu maafisa wa utawala huo wa Kizayuni na wa Marekani ambao hawakutaka kutajwa majina yao wakieleza kwamba, Washington inaandaa pendekezo jipya, ambalo litawasilishwa kwa Tel Aviv na wapatanishi, ingawa haina matumaini ya kufanikisha hivi karibuni mapatano kati ya pande mbili.
 
Kwa mujibu wa maafisa hao wa Washington na Tel Aviv, Marekani imeutaja mpango huo ambao unatayarishwa kama "pendekezo la fursa ya mwisho."
 
Kulingana na kile maafisa hao wameliambia KAN, pendekezo hilo jipya la mapatano litakalowasilishwa na Marekani linajumuisha masuala yote yanayobishaniwa, muhimu zaidi kati yao ni la Ukanda wa Philadelphia uliopo kwenye mpaka wa Ukanda wa Ghaza na Misri.

Kwa miezi kadhaa sasa, Marekani, Qatar na Misri zimekuwa zikijaribu kufanikisha makubaliano kati ya utawala wa Kizayuni wa Israel na harakati ya Hamas ili kuhakikisha mateka wa Kizayuni na wafungwa wa Kipalestina wanaachiwa huru, vita vinasitishwa na hatimaye kukomeshwa huko Ghaza na misaada ya kibinadamu kuruhusiwa kuingizwa katika eneo hilo lililowekewa mzingiro. Hata hivyo juhudi hizo za upatanishi zimekwama hadi sasa kutokana na waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni Benjamin Netanyahu kukataa takwa la msingi la Hamas la kukomesha vita.../

 

Tags