Iraq: Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani kuondoa wanajeshi wake huko Iraq katika muda wa miaka 2
Iraq imesema kuwa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani, ambao ulisalia katika nchi hiyo ya Kiarabu kwa kisingizio cha kupambana na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh miongo miwili baada ya kuivamia na kuikalia kwa mabavu nchi hiyo mwaka wa 2003, utaondoa kikamilifu wanajeshi wake ndani ya miaka miwili kuanzia sasa. Haya yameelezwa na Thabit al Abbasi Waziri wa Ulinzi wa Iraq.
Amesema, hadi kufikia Septemba mwaka kesho muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani utawaondoa wanajeshi wake katika kambi zake huko Baghdad mji mkuu wa Iraq na katika maeneo mengine ya nchi hiyo isipokuwa kaskazini kwa eneo la Kurdistan na kwamba wanajeshi wa Marekani wataondoka katika eneo la Kurdistan ifikapo mwezi Septemba mwaka 2026.
Waziri wa Ulinzi wa Iraq amesema kuwa Waziri mwenzake wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin ameeleza kuwa miaka miwili haitoshi kutekeleza uondoaji huo wa wanajeshi wai Marekani huko Iraq na kwamba Baghdad imekataa pendekezo la Austin kuhusu kuongezewa mwaka mmoja kusalia huko Iraq.
Jana Jumapili Waziri Mkuu wa Iraq Shia al Sudani alisema kuwa nchi hiyo imechukua hatua muhimu za kulipatia ufumbuzi suala la kuendelea kusalia Iraq muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani. Al Sudani pia amevipongeza vikosi vya usalama vya Iraq akisema vimefanikiwa kudumisha amani na utulivu huko Iraq na akasema hawatasita kukamilisha mchakato wa kujitawala Iraq.