Tiketi za ndege zaadimika 'Israel', wengi wanatoroka baada ya makombora ya Iran kutua
(last modified Thu, 03 Oct 2024 12:33:15 GMT )
Oct 03, 2024 12:33 UTC
  • Tiketi za ndege zaadimika 'Israel', wengi wanatoroka baada ya makombora ya Iran kutua

Kufutwa na kuakhirishwa safari za ndege na makampuni ya Ulaya kwenda na kutoka 'Israel' kufuatia hatua ya Iran kuvurumisha makombora dhidi ya ngome za kijeshi na kijasusi za utawala ghasibu wa Israel kumefanya tiketi za ndege kuwa ghali na adimu.

Kwa mujibu wa gazeti la kiuchumi la Kiibrania la Calcalist, kupata tiketi ya kuondoka Tel Aviv imekuwa kazi isiyowezekana, kufuatia hatua ya kijeshi ya Iran ya kuvurumisha makombora ya kulipiza kisasi dhidi ya utawala wa Kizayuni.  Hayo yanajiri sanjari na siku kuu ya Kiyahudi ya Rosh Hashanah ambayo inaadhimishwa Ijumaa ambayo kwa kawaida huandamana na mahitaji ya usafiri.

Idadi kubwa ya watu ambao sasa wanataka kutoroka Israel haijawahi kushuhudiwa huku  Wakala wa Usalama wa Anga katika Umoja wa Ulaya ukiamuru makampuni ya ndege yaache kuruka hadi Israel hadi mwisho wa Oktoba.  Baadhi ya makampuni ya ndege ya Ulaya yemetangaza kufuta safari zao Israel hadi mwezi Disemba.

Kwa mujibu wa ripoti ya Calcalist, hata kabla ya kuuawa kwa Katibu Mkuu wa Hizbullah Hassan Nasrallah wiki iliyopita, sekta ya usafiri wa anga nchini Israel ilikuwa katika hali mbaya, huku idadi kubwa ya makampuni ya kigeni yakisimamisha safari za ndege kwenda na kutoka Israel kufuatia operesheni za kijeshi za Hizbullah.

Ripoti hiyo inaonyesha hatua ya mashirika ya ndege ya Ulaya kufuta safari Israel imepelekea tasnia ya usafiri wa anga katika utawala huo kuvurugika kabisa.

Hayo yanajiri wakati ambapo kwa mujibu wa gazeti la Kiiberania la  Yediot Aharonoth, uchumi wa Israel unatarajiwa kukua kwa 0% mwaka wa 2024 na huku utawala wa Kizayuni wa Israel ukikumbwa na nakisi ya bajeti ya 9%.