Sababu za kushindwa utawala wa Kizayuni huko Lebanon
(last modified Fri, 25 Oct 2024 02:37:42 GMT )
Oct 25, 2024 02:37 UTC
  • Sababu za kushindwa utawala wa Kizayuni huko Lebanon

Ikiwa zimepita siku 32 tangu utawala wa Kizayuni uanzishe mashambulizi makubwa na ya pande zote dhidi ya Lebanon, lakini Tel Aviv hadi sasa imegonga mwamba na kushindwa kutimiza malengo yake nchini humo.

Utawala wa Kizayuni ulianzisha mashambulizi makubwa dhidi ya Lebanon tangu siku 32 zilizopita. Utawala huo mwaka mmoja uliopita pia ulitekeleza hujuma za kijeshi dhidi ya Lebanon hata hivyo hujuma hizo zimeshtadi pakubwa tangu siku 32 zilizopita na zimekuwa za pande zote. Sayyid Hassan Nasrullah Katibu Mkuu wa Harakati ya Muqawama ya Lebanon Hizbullah na viongozi pamoja na makamanda kadhaa wa harakati hiyo wameuawa shahidi katika mashambulizi hayo ya kinyama ya utawala wa Kizayuni. Utawala wa Kizayuni umeyaweka katika ajenda yake ya kazi malengo eti ya kuidhoofisha Lebanon, kuipokonya silaha nchi hiyo, kuwarudisha nyuma wanamuqawama hadi katika mipaka ya Mto Litani ili kuwawezesha  wanajeshi wake wasonge mbele kusini mwa Lebanon na pia kuibua mizozo ya kimadhehebu na fitna huko Lebanon lakini malengo yote haya yamefeli na kugonga mwamba licha ya kuuliwa shahidi Sayyid Hassan Nasrullah  na makamanda wa harakati ya Hizbullah. 

Moja ya sababu za kushindwa utawala wa Israel huko Lebanon ni hii kuwa kinyume na ulivyotarajia utawala huo, harakati ya muqawama ya Lebanon Hizbullah si tu haijasambaratika baada ya kuuliwa kigaidi Sayyid Hassan Nasrullah bali imeshadidisha mashambulizi yake dhidi ya utawala wa Kizayuni na ndani kabisa ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel). Muqawama wa Kiislamu wa Lebanon kila siku unaushambulia kwa makombora na ndege zisizo na rubani (droni) mji wa Haifa na nje ya mji huo ambao ni makao makuu ya kimkakati ya kiviwanda na kistratejia ya utawala wa Kizayuni. Makombora ya Hizbullah yamefika kaskazini mwa mji wa Haifa yakiwa yamevurumishwa kutoka umbali wa kilomita 20 kaskazini mwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu. Kwa hakika  Hizbullah imezidisha mpaka wa makombora yake na hali ya wasiwasi kwa Wazayuni kutokana na mashambulizi yao ya kikatili dhidi ya Lebanon ili kuwazidishia mashinikizo. 

Hizbullah ya Lebanon yavurumisha makombora katika mji wa Haifa 

Sababu nyingine muhimu ni kuwa utawala wa Kizayuni imeshindwa pia katika vita vya nchi kavu dhidi ya Lebanon kwa sababu vikosi vya nchi kavu vya harakati ya Hizbullah, ni vikosi vilivyofunzwa vyema na vinavyojua vita vya msituni ambavyo katika muongo mmoja uliopita pia vilipata mafunzo makubwa huko Syria  katika vita dhidi ya magaidi wa Daesh. Ni wazi kuwa, kushindwa utawala wa Kizayuni katika vita vya nchi kavu na kuingia Lebanon kupitia njia ya ardhini ni sababu kuu nyingine ya kushindwa utawala huo nchini humo. 

Sababu nyingine kuu pia ni kwamba kuuawa shahidi Sayyid Hassan Nasrullah hakujaisambaratisha harakati ya Hizbullah ya Lebanon bali kumezidisha irada na azma ya wanamuqawama wa Hizbullah kwa ajili ya kupambana na utawala wa Kizayuni na kulipiza kisasi mauaji ya Katibu Mkuu wake. Ni dhahir shahir kuwa kwa upande wa kisaikolojia wanamuqawama wa Hizbullah wako katika hali ya mlingano na wameweza kujihuisha upya na kutekeleza mikakati yake mkabala wa Wazayuni. 

Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon 

Sababu nyingine muhimu inayotajwa kuhusiana na suala hilo ni tajiriba ya kihistoria ya Wazayuni inayonyesha kuwa katika miongo iliyopita wanajeshi wa Kizayuni wamepata vipigo mtawalia kutoka kwa wanamuqawama wa Hizbullah ya Lebanon. Hossein Al-Jashi, mwakilishi katika Bunge la Lebanon kutoka mrengo wa "Loyalty to the Resistance" ameashiria njama za miaka 30 za Wazayuni za kutaka kuuangamiza muqawama wa Lebanon na kusema: 'Wazayuni waliamua kuiangamiza Hizbullah katika kikao cha mwaka 1996 huko Sharm el-Sheikh kufuatia makubaliano yaliyofikiwa kati ya Marekani na Ufaransa hata hivyo mwaka 2000, waliondoka Lebanon baada ya kupata kipigo cha muqawama. Adui Mzayuni kwa mara nyingine tena mwaka 2006 alijaribu kuingamiza harakati ya Hizbullah hata hivyo aligonga mwamba.'

Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni amezungumzia kuhusu mfumo mpya katika eneo la Asia Magharibi baada ya kuuliwa shahidi Sayyid Hassan Nasrullah Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon lakini wanajeshi wa utawala huo wameshindwa kukabiliana na wanamapambano wa Lebanon baada ya kuanza mapigano ya pande zote ya nchi kavu.