Bobi Wine: Nitapitia upya mikataba ya mafuta ya Uganda iwapo nitachaguliwa Rais
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i135254-bobi_wine_nitapitia_upya_mikataba_ya_mafuta_ya_uganda_iwapo_nitachaguliwa_rais
Bobi Wine mgombea mkuu wa upinzani katika uchaguzi wa kiti cha urais nchini Uganda uliopangwa kufanyika wiki ijayo, amesema kuwa atapitia upya makubaliano yaliyofikiwa kati ya nchi hiyo na makampuni ya mafuta duniani iwapo ataibuka na ushindi. Amesema ataifanyia marekebisho mikataba yoyote ambayo haina manufaa na maslahi kwa watu wa Uganda.
(last modified 2026-02-15T09:07:51+00:00 )
Jan 08, 2026 12:48 UTC
  • Bobi Wine
    Bobi Wine

Bobi Wine mgombea mkuu wa upinzani katika uchaguzi wa kiti cha urais nchini Uganda uliopangwa kufanyika wiki ijayo, amesema kuwa atapitia upya makubaliano yaliyofikiwa kati ya nchi hiyo na makampuni ya mafuta duniani iwapo ataibuka na ushindi. Amesema ataifanyia marekebisho mikataba yoyote ambayo haina manufaa na maslahi kwa watu wa Uganda.

Uganda baadaye mwaka huu inatarajia kuanza uzalishaji wa mafuta yasiyosafishwa. Itakumbukwa kuwa makampuni yote ya TotalEnergies la Ufaransa na CNOOC la Uchina yanafanya kazi kwa mujibu wa mapatano yaliyofikia na serikali ya Uganda.

Bobi Wine ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi anachuana na Yoweri Museveni katika uchaguzi wa pili mfululizo baada ya kuibuka na asilimia 35 ya kura katika uchaguzi wa rais wa mwaka 202. Amesema kuwa atapitia upya mikataba yote na kwamba sehemu yoyote ndani ya mikataba hiyo ambayo haiwanufaishi wananchi itarekebishwa.

Waziri wa Habari wa Uganda na kampuni za TotalEnergies na CNOOC hadi sasa hazijatoa jibu kwa kauli hizi za Bobi Wine. 

Akiba ya mafuta ya Uganda inakadiriwa kuwa mapipa bilioni 6.65. Uganda iligundua mafuta miaka 20 iliyopita lakini uzalishaji umekuwa ukicheleweshwa mara kwa mara kutokana na kutoelewana kati ya makampuni ya kimataifa na serikali, na vilevile upinzani wa wanaharakati wa mazingira.

Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda mwenye miaka 81 amekuwa mamlakani kwa miaka 40. 

Mgombea huyo mkuu wa upinzani wa kiti cha urais nchini Uganda amesema kuwa amepigwa mara mbili na askari usalama  wakati wa kampeni na amezuiwa kufanya kampeni katika baadhi ya maeneo.