Afrika Kusini: Hatutazuia mpango wa Washington wa kuwapa hifadhi wazungu waliowachache
-
Cyril Ramaphosa na Trump
Afrika Kusini imesema haitapinga mpango wenye utata wa serikali ya Washington wa kuwapeleka Marekani raia wazungu walio wachache wa Afrika Kusini.
Afrika Kusini ilitoa hakikisho hilo katika mkutano wa faragha uliofanyika Desemba 23 mwaka jana baada ya kushtadi mivutano baina ya pande mbili kufuatia hatua ya mamlaka za Afrika Kusini ya kuvamia kituo cha kushughulikia watu wanaotaka kuomba hifadhi Marekani huko Johannesburg na kuwaweka kizuizini kwa muda maafisa wa Marekani na kuwakamata wakandarasi.
Muhtasari wa mkutano huo ulieleza kuwa: Maafisa wa Afrika Kusini wameiambia Washington kwamba wanakanusha madai kwamba Waafrika Kusini wazungu wanakabiliwa na mauaji ya kimbari, lakini hawezi kuzuia haki yao ya kuhajiri.
Mpango huo ulizinduliwa na Rais Donald Trump baada ya kusimamisha uandikishwaji wa aghalabu ya wakimbizi duniani, akiwapa kipaumbele wazungu walio wachache wa Afrika Kusini ambao anadai wanakabiliwa na mateso ya kubaguliwa; madai ambayo Pretoria imeyakadhibisha vikali.
Uhusiano kati ya Marekani na Afrika Kusini umezidi kuwa mbaya katika miezi ya hivi karibuni, hasa baada ya Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini kukabiliana na Trump kuhusu madai ya uongo ya mauaji ya kimbari ya wazungu na baada ya Washington kuizuia Afrika Kusini kushiriki katika mikutano ijayo ya G20.