HAMAS yalaani kimya cha walimwengu baada ya Israel kuvamia hospitali na kuua watoto ndani yake
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imesema jumuiya na taasisi za kimataifa zinabeba dhima ya kisiasa na kimaadili kwa jinai zinazoendelea kufanywa na utawala dhalimu wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza.

Hamas ilisema uvamizi dhidi ya Hospitali ya Kamal Adwan umefanywa "saa chache baada ya kuiwekea mzingiro" hospitali hiyo, kitendo ambacho kilifuatiwa na kukamatwa na kunyanyaswa wagonjwa, majeruhi, wafanyikazi wa kada ya tiba, familia zilizohamishwa, na wanaharakati wa vyombo vya habari, ambao walipelekwa mahali kusikojulikana.
Harakati hiyo ya Muqawama ya Palestina imeendelea kubainisha katika taarifa yake kwamba, utawala dhalimu wa Kizayuni unaendeleza mauaji ya kimbari kaskazini mwa Ghaza, bila kujali matokeo yake, huku ukisaidiwa na kuungwa mkono kikamilifu na utawala wa Marekani.
Hamas imemalizia taarifa yake yake kwa kutoa wito kwa nchi za Kiislamu, yakiwemo mataifa ya Kiarabu kuwajibika kwa kwenda mbali zaidi ya kutosheka na kutoa kauli tupu za kulaani, kwa kuchukua hatua ili kukomesha mauaji ya kimbari na maangamizi ya kizazi ambayo yamekuwa yakifanywa dhidi ya Wapalestina.../