Israel yaibembeleza Iran isijibu mashambulizi
(last modified Sat, 26 Oct 2024 10:04:18 GMT )
Oct 26, 2024 10:04 UTC
  • Israel yaibembeleza Iran isijibu mashambulizi

Duru tatu za Magharibi zimedai kuwa, kabla ya kufanya shambulizi nchini Iran, utawala wa Kizayuni ulituma ujumbe kwa Iran ukiibembeleza Jamhuri ya Kiislamu isijibu mashambulizi hayo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, mtandao wa Axios wa Marekani umezinukuu duru za kuaminika na kusema kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel jana Ijumaa na kabla ya kufanya mashambulizi nchini Iran iliomba Iran isijibu mashambulizi hayo.

Duru hizo zmedai kuwa, ujumbe wa utawala wa Kizayuni kwa hakika ni jaribio la utawala huo la kuzuia majibizano ya mashambulio kati ya Israel na Jamhuri ya Kiislamu na eti kuzuia mvutano mkubwa zaidi. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ujumbe wa utawala wa Kizayuni umewasilishwa kwa Iran kupitia pande kadhaa.

Awali serikali za Marekani na Uingereza pia ziliiomba Iran isijibu shambulizi na uchokozi huo.   

Televisheni ya Al Jazeera ya Qatari imemnukuu afisa wa ngazi ya juu wa Marekani akithibitisha kumalizika mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran na kuandika kuwa, tunaiomba Tehran isijibu mashambulizi hayo.

Hata hivyo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza kuwa inalinda haki yake ya kujibu uchokozi huo kwa mujibu wa Hati ya Umoja wa Mataifa na jukumu lake la kulinda ardhi na maslahi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.