Jeshi la Yemen: Tutaendelea kupiga meli zote zenye uhusiano na Israel
Msemaji wa jeshi la Yemen amesema kuwa, jeshi hilo litaendelea kuzipiga meli zote zenye uhusiano na Israel katika maji ya karibu na Yemen, bila ya kujali bendera na wamiliki wa vyombo hivyo vya baharini.
Brigedia Jenerali Yahya Saree alisema hayo jana Jumapili na kusisitiza kuwa, makampuni mengi ya meli yenye uhusiano na Israel yanajaribu kukwepa adhabu zinazotolewa na Yemen kwa kuuza hisa zao kwa makampuni mengine au kubadilisha usajili wa meli hizo lakini vikosi imara vya ulinzi vya Yemen havitojali ujanja na hila hizo za Kizayuni, bali vitaendelea kukipiga chombo chochote cha baharini chenye uhusiano na Israel.
Jenerali Saree ameongeza kuwa, pande zote zinazohusika na kampuni na meli hizo zimo kwenye orodha ya adhabu na marufuku ya kuvuka eneo la operesheni la Jeshi la Yemen.
Amesema: "Taarifa za kijasusi zinathibitisha kwamba makampuni mengi ya adui Israel yanafanya kazi ya kuuza hisa zao na kuhamisha hati miliki za meli zao kwa makampuni mengine au kuzisajili kwa majina tofauti kama njia ya kukwepa adhabu na marufuku zilizowekwa na Jamhuri ya Yemen. Lakini Yemen itaendeleza marufuku hizo na itaendelea kuzipiga meli hizo hadi utawala wa Kizayuni utakapokomesha jinai zake huko Ghaza na Lebanon.
Vikosi vya ulinzi vya Yemen vimeshafanya mamia ya mashambulizi ya makombora dhidi ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Israel na dhidi ya meli za utawala wa Kizayuni bali dhidi ya chombo chochote cha baharini kinachoelekea Israel tangu mwezi Oktoba 2023. Operesheni hizo zinaendelea kuusababishia utawala wa Kizayuni hasara kubwa isiyofidika.