Syria yajibu madai ya Netanyahu kuhusu Golan inayokaliwa kwa mabavu
Spika wa Bunge la Syria amejibu madai ya kijeuri ya Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel kuhusu Golan inayokaliwa kwa mabavu.
Hammouda Youssef Sabbagh, Spika wa Bunge la Syria, alitangaza jana Jumanne kwamba madai ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kuhusu Golan inayokaliwa kwa mabavu hayana umuhimu na kwamba Golan inatambuliwa kuwa sehemu ya ardhi ya Syria.
Kuhusiana na hali ya sasa ya ndani ya nchi hiyo, Sabbagh pia amesema: Bunge linanyoosha mkono wa ushirikiano kwa watawala wapya wa Syria na linajitambua kuwa mtumishi wa watu.
Siku ya Jumapili iliyopita, kufuatia kuanguka serikali ya Syria, vyombo vya habari vya Israel vilitangaza kuwa vifaru vya jeshi la utawala huo vimewasili katika Miinuko ya Golan inayokaliwa kwa mabavu.
Baada ya hapo Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni alisema, Miinuko ya Golan ya Syria inayokaliwa kwa mabavu itabaki "milele kuwa sehemu isiyoweza kutenganishwa" na Israel.
Benjamin Netanyahu alitoa tangazo hilo Jumatatu, siku moja baada ya kuwaamuru wanajeshi wa utawala huo ghasibu wasonge mbele hadi katika eneo linalotenganisha Golan na ardhi nyingine ya Syria.