Marekani yakiri kuwa na mkono katika matukio ya sasa nchini Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i120004-marekani_yakiri_kuwa_na_mkono_katika_matukio_ya_sasa_nchini_syria
Kufuatia matukio ya sasa, ya haraka na ya ghafla ya kijeshi nchini Syria na kutekwa Damascus na makundi yenye silaha na hatimaye kuondoka madarakani Rais wa Syria Bashar al-Assad, Marekani imekiri kwamba imekuwa na nafasi katika matukio hayo.
(last modified 2024-12-11T07:32:06+00:00 )
Dec 11, 2024 07:32 UTC
  • Marekani yakiri kuwa na mkono katika matukio ya sasa nchini Syria

Kufuatia matukio ya sasa, ya haraka na ya ghafla ya kijeshi nchini Syria na kutekwa Damascus na makundi yenye silaha na hatimaye kuondoka madarakani Rais wa Syria Bashar al-Assad, Marekani imekiri kwamba imekuwa na nafasi katika matukio hayo.

Katika muktadha wa malengo yake pia, Washington imezungumzia uwezekano wa kuondolewa majina ya baadhi ya makundi yenye silaha ya Syria katika orodha ya makundi ya kigaidi.

Jake Sullivan, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani, amekiri katika mahojiano na CBS kwamba nafasi ya Marekani katika matukio ya Syria si ya moja kwa moja, lakini imekuwa na nafasi na mchango katika kutayarisha mazingira ya kuondoka madarakani Bashar Assad. Sullivan amedai katika mazungumzo hayo kwamba: "Hatukushiriki moja kwa moja katika mashambulizi yaliyowafikisha waasi madarakani nchini Syria, hatukuunga mkono na hatukuwa sehemu yake. Tulikuwa sehemu ya juhudi kubwa za kikanda na kimataifa za kuwadhoofisha wafuasi wa Assad."

Jake Sullivan pia amesema kwamba: "Tutashirikiana na makundi yote nchini Syria, na kama Rais wa Marekani, Joe Biden alivyosema, makundi ya waasi yanajumuisha makundi ambayo yametambuliwa kuwa ya kigaidi. Sasa swali ni kwamba watafanya nini kuunda Syria iliyo bora zaidi."

Jake Sullivan

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Matthew Miller, amesema utawala wa Biden unatafuta njia za kushirikiana na makundi yenye silaha ya Syria ambayo yalimuondoa madarakani Bashar al-Assad na inawasiliana na washirika wake wa kikanda, kama vile Uturuki, ili kusaidia kuanza diplomasia isiyo rasmi. Ameongeza kuwa Washington ina njia za mawasiliano na makundi mbalimbali, likiwemo lile lililotangazwa na Marekani kuwa kundi la "kigaidi".

Msimamo wa Marekani katika suala la nafasi ya nchi hiyo katika matukio ya hivi sasa nchini Syria kwa upande mmoja, na mawasiliano ya Washington na baadhi ya makundi yenye silaha, hususan Hay'at Tahrir al-Sham, ni viashiria vya malengo halisi ya Marekani na mienendo yake ya kinafiki na kiindumakuwili. 

Tangu mwaka 2011, Syria iliingia katika mgogoro na machafuko yaliyoanzishwa na makundi yanayoungwa mkono na nchi za Magharibi na washirika wake wa Kiarabu pamoja na Uturuki, na hatua kwa hatua makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na Marekani, Uingereza, Ufaransa na washirika wao wa kikanda yakaingia vitani na serikali halali ya nchi hiyo kwa nia ya kubadilisha mlingano wa nguvu wa kieneo kwa maslahi ya Israel na kudhoofisha Kambi ya Muqawama. Baada ya msaada wa kijeshi wa Iran na Russia kwa ombi la serikali halali ya Syria, vikundi hivyo vya kigaidi vilikandamizwa na hatimaye, chini ya uungaji mkono wa Uturuki, vilipelekwa katika mkoa wa Idlib, kaskazini magharibi mwa Syria. Kuanzia tarehe 27 mwezi uliopita wa Novemba, 2024, kwa msaada wa baadhi ya nchi, haswa Uturuki, na msaada wa vikosi vipya vya wapiganaji wa kigeni, vikundi hivyo vyenye silaha vilianzisha mashambulizi makubwa dhidi ya kambi na ngome za jeshi la Syria kaskazini magharibi, magharibi na kusini magharibi mwa Aleppo. Hatimaye, majuzi Desemba 8, 2024, Kamandi ya Jeshi la Syria ilitangaza kuanguka kwa serikali ya Bashar al-Assad. Sasa makundi yenye silaha yanayoongozwa na Abu Muhammad al-Jolani, mkuu wa kundi la Tahrir al-Sham, yamechukua utawala wa Syria.

Nukta muhimu ya kuashiriwa hapa ni kwamba, Marekani ambayo hapo awali ililiweka kundi la Hay'at Tahrir al-Sham katika orodha ya makundi ya kigaidi, sasa imebadili msimamo wake na inazungumzia uwezekano wa kuliondoa jina la kundi hilo katika orodha ya magaidi! Katika muhula wake wa kwanza wa urais, Donald Trump aliliweka kundi hilo katika orodha ya makundi ya kigaidi.

Donald Trump

Rais wa Marekani, Joe Biden, pia alisema Jumapili usiku kwamba: "Tutashirikiana na makundi yote ya Syria, ikiwa ni pamoja na yale yaliyo katika mchakato unaoongozwa na Umoja wa Mataifa, kwa ajili ya kuhama kutoka utawala wa Assad kuelekea kwenye Syria huru yenye katiba mpya!!"

Kwa utaratiibu huo, hivi sasa Washington iko tayari kuondoa majina ya makundi hayo katika orodha ya makundi ya kigaidi ikiwa ni njia ya kuitambua rasmi serikali mpya, baada ya makundi yenye silaha yanayokwenda sambamba na malengo na sera za Marekani kutwaa madaraka nchini Syria. Inaweza kutabiriwa kuwa nchi zingine za Magharibi, haswa Uingereza, pia zitafuata mkondo huo huo.