Waziri wa Lebanon: Israel imefanya uhalifu wa kivita wa kimazingira
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i120108-waziri_wa_lebanon_israel_imefanya_uhalifu_wa_kivita_wa_kimazingira
Waziri wa Mazingira wa Lebanon amesema kuwa Israel imeharibu ardhi na misitu ya kusini mwa hiyo kwa kutumia silaha zilizopigwa marufuku.
(last modified 2024-12-14T02:28:35+00:00 )
Dec 14, 2024 02:28 UTC
  • Waziri wa Lebanon: Israel imefanya uhalifu wa kivita wa kimazingira

Waziri wa Mazingira wa Lebanon amesema kuwa Israel imeharibu ardhi na misitu ya kusini mwa hiyo kwa kutumia silaha zilizopigwa marufuku.

Nasser Yassin, Waziri wa Mazingira wa Lebanon ameongeza kuwa, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel limeteketeza kwa makusudi na kuharibu hekta 5,745 za ardhi na misitu kusini mwa Lebanon wakati wa vita kwa kutumia silaha zilizopigwa marufuku kama fosforasi nyeupe.

Waziri wa Mazingira wa Lebanon ameongeza kuwa: Kiwango hicho ni kwa uchache mara 4 ya uharibifu uliosababishwa kwenye misitu na malisho yaliyoteketezwa kwa moto huko Lebanon katika miaka ya hivi karibuni.

Akisisitiza kwamba hivi sasa miji na vijiji 52 vya Lebanon vimeharibiwa kutokana na mashambulizi ya jeshi la Israel, na wakazi wake hawawezi kurejea katika miji na vijiji hivyo, Nasser Yassin amesema kuwa bado kuna sehemu kubwa za ardhi ya Lebanon ambayo inakaliwa kwa mabavu na jeshi la Kizayuni.

Makubaliano ya kusitisha vita kati ya utawala wa Kizayuni wa Israel na Lebanon, chini ya upatanishi wa kimataifa, yalianza kutekelezwa asubuhi ya Jumatano ya tarehe 27 Novemba 2024, lakini tangu wakati huo, jeshi la utawala wa Kizayuni limekuwa likikiuka mara kwa mara makubaliano hayo na kuzuia kurejea wakimbizi wa Lebanon katika baadhi ya miji na vijiji kusini mwa nchi hiyo.