Afisa wa UN: Ni vigumu kupeleka misaada Gaza
(last modified Wed, 25 Dec 2024 03:35:03 GMT )
Dec 25, 2024 03:35 UTC
  • Afisa wa UN: Ni vigumu kupeleka misaada Gaza

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa imekuwa vigumu kufikisha hata msaada mdogo kwa raia wa Palestina huko Ukanda wa Gaza.

Thomas Fletcher jana alieleza kuwa katika mwaka mmoja uliopita idadi kubwa ya wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu wameuawa  Ukanda wa Gaza; na hivyo kuwa vigumu kufikisha hata sehemu ya misaada inayohitajika kwa ajili ya wakazi wa ukanda huo licha ya mahitaji makubwa ya kibinadamu.

Fletcher ameongeza kuwa: Wanajeshi wa Israel wanaendelea kuwazuia wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu kufikisha misaada kwa wakazi wa Gaza. 

Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa Anayehusika na Masuala ya Kibinadamu amesisitiza licha ya kuwa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) imetoa maamuzi kadhaa ya muda mkabala wa jinai za kivita za mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza lakini uhalifu unaoendelea unaonyesha kuwa hakuna mahali salama kwa watu huko Gaza, huku shule  hospitali na miundombinu ya mji huo ikiwa imebomolewa na kuharibiwa.

Hii ni katika hali ambayo ofisi ya habari ya Palestina pia imetangaza kuwa utawala ghasibu wa Kizayuni umekusudia kuwasababishia njaa raia wa Kipalestina na kusababisha hali ngumu ya kiuchumi kwa kuunga mkono kikamilifu wizi wa misaada ya kibinadamu na kuwashambulia wafanyakazi wa sekta hiyo.