NGO: Israel inashikilia miili ya Wapalestina 198 waliouawa mwaka 2024
(last modified Wed, 01 Jan 2025 13:02:18 GMT )
Jan 01, 2025 13:02 UTC
  • NGO: Israel inashikilia miili ya Wapalestina 198 waliouawa mwaka 2024

Kampeni ya Kitaifa ya Kurejesha Miili ya Mashahidi (The National Campaign to Retrieve Martyrs' Bodies) imeeleza kuwa viongozi wa utawala ghasibu wa Israel wanashikilia miiili ya mashahidi wa Kipalestina 198 walisajiliwa mwaka jana wa 2024.

Kundi hilo limeeleza kuwa idadi hiyo ni sawa na theluthi moja ya miili ya mashahidi inayoshikiliwa katika makaburi ya siri na mochwari za Israel. 

Hayo ni makaburi yasiyo na alama yaliyopakana na mawe, kila moja likiwa na bamba la chuma lenye nambari badala ya jina la marehemu. Nambari hizo zinakwenda sambamba na faili la mtu binafsi zinazohifadhiwa na mamlaka husika ya usalama ya Israel.

Mwezi Septemba mwaka 2019, Mahakama Kuu ya Israel ilitoa uamuzi kwamba makamanda wa kijeshi wa utawala huo wanaweza kuzuia kwa muda miili ya Wapalestina waliouawa na wanajeshi wa utawala huo ili iweze kutumika kama turufu katika mazungumzo ya mapatano ya siku za usoni.

Kampeni ya Kitaifa ya Kurejesha Miili ya Mashahidi wa Kipalestina pia imeeleza kuwa idadi hiyo haijumuishi miili iliyozuiliwa na Israel kutoka Ukanda wa Gaza kutokana na ukosefu wa taarifa sahihi.

Jeshi la Israel linaendeleza vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza ambavyo hadi sasa vimeuwa Wapalestina zaidi ya 45,000 wengi wao wakiwa wanawake na watoto wadogo. Utawala wa Kizayuni unaendeleza jinai hizo licha ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutaka kusitishwa haraka iwezekanavyo mauaji hayo.