UNIFIL yasisitiza kuondoka Lebanon wanajeshi wa Israel
(last modified Mon, 27 Jan 2025 07:08:01 GMT )
Jan 27, 2025 07:08 UTC
  • UNIFIL yasisitiza kuondoka Lebanon wanajeshi wa Israel

Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kusini mwa Lebanon (UNIFIL) kimetaka kuondoka kikamilifu wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel huko kusini mwa Lebanon.

Kikosi hicho kimetoa taarifa na kueleza kuwa kimepata wasiwasi mkubwa kufuatia taarifa za raia wa Lebanon wanaorejea katika vijiji vyao ambako jeshi la Israel bado lipo na maafa yaliyosababishwa na mashambulizi ya Israel dhidi ya raia hao. 

Wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa huko kusini mwa Lebanon wamesisitiza kuwa kuna udharura wa kutekelezwa azimio nambari 1701 la Baraza la Usalama la UN na kutahadharisha kuwa kushtadi mivutano ni tishio kwa  hali ya usalama inayolegalaga huko Lebanon.

Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel limekiuka makubaliano ya kusimamisha vita kwa kuwashambulia raia wa Lebanon ambao walikuwa njiani wakirejea majumbani kwao katika maeneo ya kusini mwa nchi hiyo.

Wizara ya Afya ya Lebanon imeripoti kuwa, tangu jana asubuhi hadi sasa Walebanoni 10 wameuawa shahidi na wenegine 83 kujeruhiwa katika mashambulizi ya utawala wa Kizayuni nchini humo.