Mash'al: Upo udharura kwa Wapalestina kuwa kitu kimoja
Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amesisitiza kuwa damu za mashahidi wa Kipalestina zinatilia mkazo kuwepo umoja kwa lengo la kupambana na adui Mzayuni.
Khalid Mash'al amesema ujumbe wa Hamas ni kwa ajili ya kupatikana umoja, kusambaratisha undumakuwili, kuboresha hali ya mambo ya ndani na kufanikisha umoja wa kitaifa. Mash'al amesema hii ni kwa sababu Wapalestina hawawezi kupata ushindi iwapo hawatakuwa na umoja na mshikamano.
Mash'al ameongeza kuwa wananchi wa Palestina wanapigania haki zao, ardhi na matukufu yao na hawataacha kufanya juhudi hadi hapo malengo na matakwa yao yote yatakapotimia.
Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas amesema hali ya mambo katika nchi za Kiislamu, Kiarabu na eneo zima la Mashariki ya Kati imewafanya walimwengu wasahau kadhia ya Palestina.
Amesema hali hiyo inapasa kubadilishwa na kwa mara nyingine tena amewatole wito walimwengu kufanya juhudi za kuipa umuhimu kadhia ya Palestina na kuifanya kuwa kadhia muhimu inayoihusu Umma wa Kiislamu.