Cuba: Gaza ni mali ya wananchi wa Palestina
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Cuba imetangaza kuwa, inaunga mkono kikamilifu Palestina na kwamba, Gaza ni mali ya wananchhi wa Palestina.
Taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni imetolewa baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kutangaza hadharani kwamba Washington itatwaa na kuchukua udhibiti wa Ukanda wa Gaza katika mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, mjini Washington.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Cuba amesisitiza katika taarifa rasmi kwamba Cuba inaunga mkono kwa dhati kadhia ya Palestina na inalaani jaribio lolote la kubadilisha muundo wa idadi ya watu wa eneo hilo.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Cuba amebainisha kwamba, njia pekee inayowezekana ya kumaliza mzozo wa sasa ni kutambuliwa kwa taifa huru la Palestina kwenye mipaka ya kabla ya 1967 na Quds Mashariki ukiwa mji mkuu wake.
Katika sehemu nyingine ya matamshi yake hayo, Bruno Eduardo Rodríguez Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Cuba amesisitiza kuwa, Gaza ni mali ya watu wa Palestina na kwamba, Israel na muungaji mkono wake yaani Marekani wanapaswa kudiriki na kuheshimu hilo.
Viongozi wa Cuba wamekuwa wakiukosoa mara kwa mara ukatili wa utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina na pia wametaka kumalizika kwa vita vya Gaza na kusitishwa mauaji ya raia wa Gaza. Hivi karibuni, serikali ya Cuba ilitangaza kuwa, kama sehemu ya dhamira yake ya dhati ya kusaidia juhudi halali za kimataifa za kumaliza mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Palestina, imejiunga na kesi ya Afrika Kusini dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki.