Kufichuka nia halisi ya utawala wa Kizayuni nchini Syria
Kimya na kutochukua hatua yoyote watawala wapya wa Syria vimeufanya utawala wa Kizayuni wa Israel ufikirie kuyatwaa kabisa maeneo mapya yaliyokaliwa kwa mabavu nchini Syria.
Gazeti la Kizayuni la Haaretz limeripoti kwamba, jeshi la Israel limeanzisha vituo saba vya kijeshi katika maeneo mapya yanayokaliwa kwa mabavu katika ardhi ya Syria. Vituo hivyo vinaanzia katika eneo la ukanda wa Jabal Al-Sheikh kaskazini hadi Tal Qudna katika pembetatu ya mpaka kati ya Syria, Jordan na Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Tangu baada ya kuanguka serikali ya Assad, jeshi la Israel limevuka mpaka kati ya Milima ya Golan inayokaliwa kwa mabavu na ardhi nyingine ya Syria na kutwaa maeneo ya karibu na Golan katika majimbo ya Daraa na Quneitra. Hatua hii imechukuliwa baada ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kutupilia mbali makubaliano ya mwaka 1974 kati ya Syria na utawala wa Israel kuhusu Milima ya Golan. Redio ya Jeshi la Israel pia imetangaza kuwa baraza la mawaziri la utawala huo ghasibu limeafiki kukalia kwa mabavu eneo la "Jabal Al-Sheikh" la Syria na kuanzisha ukanda wa kutenganisha maeneo hayo na ardhi ya Syria.
Mnamo Mei 31, 1974, Syria na utawala wa Israel zilitia saini makubaliano yanayojulikana kama Mwisho wa Mivutano baada ya kusitishwa mapigano kwa miezi 7 na Vita vya Oktoba 1973. Mkataba huo ulitiwa saini kati ya jeshi la Syria na jeshi la Israel, mbele ya wawakilishi wa Umoja wa Mataifa, Umoja wa Kisovieti na Marekani, na kwa kuzingatia azimio nambari 338 la Umoja wa Mataifa, tarehe 22 Oktoba mwaka huo. Makubaliano hayo yalitekelezwa chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa na lengo lake kuu lilikuwa kuunda ukanda usio na silaha kati ya majeshi hayo mawili, unaosimamiwa na Syria na UN.

Hivi sasa kufuatia matukio mapya ya Syria, utawala wa Kizayuni wa Israel, ukishirikiana na baadhi ya pande na kwa idhini ya nchi za Magharibi, umechukua hatua katika fremu ya juhudi za kubadilisha sura ya eneo la Magharibi mwa Asia au kuunda kile kilichopewa jina la Mashariki ya Kati mpya.
Utawala wa Israel unakusudia kuigeuza Syria kuwa "Misri ya pili" na kulazimisha Camp David mpya kwa serikali ya Damascus baada ya Trump kushika madaraka huko Marekani. Ingawaje jeshi la Israel na baraza la mawaziri la Netanyahu wamesisitiza katika taarifa tofauti kwamba hatua za hivi karibuni huko Golan ni za muda, lakini ushahidi wa kihistoria unatilia shaka madai haya. Israel imekuwa ikitaja vitendo vyake kuwa ni hatua za muda lakini vimeendelea kwa miaka mingi au hata kuwa vya kudumu. Mfano wa wazi ni sheria ya hali ya hatari, ambayo imekuwa ikitumika tangu kuasisiwa kwa utawala bandia wa Israel mwaka 1948.
Kadhalika, baada ya kuanguka serikali ya Bashar al-Assad, jeshi la Israel limezidisha kasi ya mashambulizi yake dhidi ya miundombinu na vituo vya kijeshi vya Syria, na katika kipindi hiki limeendelea kushambulia vituo vya jeshi na kufanya mashambulizi mapya mashariki na magharibi mwa nchi hiyo. Kwa miaka mingi utawala wa Kizayuni umekuwa ukifanya jitihada za kuipokonya silaha Syria mpya hususan silaha nzito na uwezo wa anga, katika muktadha wa sera za muda mrefu za Israel za kudumisha ubora wa jeshi la utawala huo dhidi ya nchi za Kiarabu na Kiislamu.

Kwa mashambulizi yake yasiyokuwa na kifani dhidi ya miundombinu ya ulinzi na jeshi ya Syria, kuanzia viwanja vya ndege, vituo vya utafiti, maghala ya silaha, helikopta na ndege za kivita hadi kwenye meli za baharini kwenye pwani ya Latakia na Tartus, utawala wa Israel unajaribu kuigeuza Syria kuwa nchi ambayo haina ulinzi wa anga ili iweza kudhibiti anga ya Syria kwa urahisi wakati na mahali popote inapotaka.
Mashambulio makubwa yanayofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya miundombinu ya Syria na kukaliwa kwa mabavu maeneo mengine ya ardhi ya nchi hiyo vimeibua maswali mazito kwa serikali mpya ya nchi hiyo hususan Abu Muhammad al-Julani na yamezidisha uwezekano wa makundi yanayounda serikali hiyo na waungaji mkono wake, kwa kupenda au kutopenda, kutumbukia mikononi mwa utawala huo tangu mwanzo na hatimae kusaidia malengo yake ya kuikalia kwa mabavu ardhi zaidi ya Syria.