Sayyid Hassan Nasrullah alivunja kiburi cha jeshi la Israel linalodai halishindwi
Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen amesema kuwa: Sayyid Hassan Nasrullah amepata mafanikio makubwa na kuvunja kiburi na majigambo ya jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel ambalo linadai eti halishindiki.
Mahdi Al-Mashat, ameandika hayo kwenye makala maalumu chini ya kichwa cha maneno: "Katika daraja ya Bwana wa Muqawama na Shahidi wa Uislamu na kuongeza kuwa: "Bwana wa Muqawama wa Lebanon alikuwa daima baba kwa watu wote huru duniani na kiongozi na ndugu kwa watu wote wema, alikuwa ni mwenye huruma na mnyenyekevu kwenye njia ya Mwenyezi Mungu. Alifuata njia ileile ya Imam Husain (AS) hadi siku ya kuuawa kwake shahidi katika njia ya Allah na ya ukombozi wa Quds."
Rais Al-Mashat ameongeza kuwa: "Shahid Sayyid Hassan Nasrullah alifanikisha kila alichotaka katika maisha yake, alimpigisha magoti adui Israel, akaharibu nganu ya kutoshindwa jeshi la Israel, akawaunga mkono waliodhulumiwa na akasimamisha uadilifu."

Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen vile vile amesisitiza kuwa, Sayyid Nasrullah ni shahidi wa umma na ubinadamu, ni shahidi wa njia ya ukombozi wa Quds na Palestina, ni shahidi wa Lebanon na Yemen na ni shahidi wa ukweli na uadilifu na maadili yote matukufu ya ulimwengu. Amesema: Sayyid Nasrullah aliishi katika kulinda maadili ya Uislamu Mashariki na Magharibi mwa dunia.
Afisa huyo wa ngazi za juu wa Yemen amesema: "Waliodhulumiwa hawajapata msaidizi kama Sayyid Nasrullahkwa miongo kadhaa, kutoka Lebanon hadi Palestina, kutoka Bosnia hadi Afghanistan, kutoka Syria hadi Iraqi na ulimwenguni kote."