Hamas: Muqawama ni chaguo la kimkakati la ukombozi wa Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i124258-hamas_muqawama_ni_chaguo_la_kimkakati_la_ukombozi_wa_palestina
Katika kumbukumbu ya mwaka wa 21 wa kuuawa shahidi Sheikh Ahmad Yassin, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imesisitiza kwa kusema: "Tunashikamana na njia ya Sheikh Ahmad Yassin, tunalinda ardhi na matukufu yetu, na tuna imani thabiti kwamba Muqawama ni chaguo la kistratijia la kujikomboa na kupata uhuru wetu."
(last modified 2026-05-20T03:07:53+00:00 )
Mar 23, 2025 03:03 UTC
  • Hamas: Muqawama ni chaguo la kimkakati la ukombozi wa Palestina

Katika kumbukumbu ya mwaka wa 21 wa kuuawa shahidi Sheikh Ahmad Yassin, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imesisitiza kwa kusema: "Tunashikamana na njia ya Sheikh Ahmad Yassin, tunalinda ardhi na matukufu yetu, na tuna imani thabiti kwamba Muqawama ni chaguo la kistratijia la kujikomboa na kupata uhuru wetu."

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Tasnim, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas imesisitiza hayo katika taarifa yake jana Jumamosi kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuuawa shahidi Sheikh Ahmad Yassin na kusema: Leo ni mwaka wa 21 wa kuuawa shahidi Sheikh Ahmad Yassin, muasisi wa harakati ya Hamas mauaji ya kikatili ambayo yalifanywa na utawala wa Kizayuni.

Kumbukumbu hizi zinawakumbusha wananchi wa Palestina maisha na njia yake, ambayo ilikuwa kama chuo na mwalimu aliyeshikamana na mafundisho ya Mwenyezi Mungu kwao, na kuwapa msukumo wa kushikamana na haki, kusimama kidete juu ya ardhi, uvumilifu, subira, kujitolea muhanga na kuihami kiume ardhi na maeneo matakatifu.

Sheikh Ahmad Yassin, mwasisi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS

 

Taarifa hiyo inaongeza kuwa: "Mauaji ya Sheikh Ahmad Yassin na viongozi wetu wengine wa kitaifa ambao ni nembo kwa taifa leo hayajawahi kutuvunja moyo na kamwe hayatavunja nia ya taifa letu ya kusimama imara katika Muqawama." Adui Mzayuni hataweza kututoa katika ardhi yetu au kufuta kadhia ya Palestina kupitia jinai na ugaidi wake. Badala yake, uhalifu huu huongeza nia, imani thabiti na kujitolea muhanga katika njia ya haki na tutazidi kushikamana na Muqawama kwani ndilo chaguo letu la kimkakati la kupigania haki na ukombozi wa ardhi yetu.

Taarifa hiyo ya HAMAS imeendelea kusema: "Mbegu iliyobarikiwa ambayo Sheikh Yassin aliipanda katika ardhi ya Palestina imejaa mapenzi kwa ardhi, kujitolea na imani thabiti juu ya uhuru na ukombozi wa ardhi ya Palestina." Mbegu hiyo imetia nguvu na kuleta uvumilivu usio na kifani katika hatua zote za mapambano na Muqawama, na mfano wa hivi karibuni zaidi ni huu Muqawama na uvumilifu unaooneshwa na wananchi wa Palestina baada ya Operesheni ya Kimbunga cha al Aqsa." Vita hivi ni mfano mashuhuri wa subira, kujitolea mhanga, ustahimilivu na kutotetereka katika historia ya zama hizi.