UNRWA: Mzingiro wa Israel utasababisha baa kubwa la njaa Gaza
Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi wa Palestina (UNRWA) ametahadharisha kwamba hatua ya utawala wa Israel ya kuweka mzingiro na kuzuia misaada ya kibinadamu kuingia katika Ukanda wa Gaza inapelekea eneo hilo la pwani kukaribia baa kubwa la njaa.
Philippe Lazzarini ameyasema hayo hayo katika chapisho kupitia mitandao ya kijamii, ambapo amesisitiza kwamba mzingiro huo, ambao unazuia chakula, dawa, maji na mafuta kuingia katika eneo hilo, umeendelea kwa muda mrefu.
Israeli imezuia kuingia kwa misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza tangu Machi 4, kufuatia kumalizika kwa awamu ya kwanza ya mapatano ya kusitisha mapigano na makubaliano na harakati ya Muqawama ya Hamas kuhusu kubadilishana mateka wa Israel kwa wafungwa wa Kipalestina.
Lazzarini amesema kila siku inayopita bila kuingia kwa msaada ina maana watoto wengi wanakwenda kulala wakiwa na njaa, magonjwa yanaenea na ukosefu wa bidhaa unazidi kuwa mbaya.
Afisa huyo mwandamizi wa Umoja wa Mataifa amesema: “Kila siku bila chakula ina maana Gaza inakaribia baa kubwa la njaa." Lazzarini amesema kuzuia msaada ni adhabu ya pamoja kwa watu wa Gaza – ambao wengi wao ni watoto, wanawake na wanaume wa kawaida.
Chini ya himaya kamili ya Marekani na washirika wake wa Magharibi, utawala haramu wa Israel ulianzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza mnamo Oktoba 7, 2023, baada ya harakati ya Muqawama ya Hamas kufanya operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa dhidi ya utawala wa Israel kama jibu kwa kampeni yake ya muda mrefu ya jinai dhidi ya Wapalestina.
Mashambulizi ya kikatili ya utawala huo dhidi ya Gaza hadi sasa yameua Wapalestina wasiopungua 50,021, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto, na kujeruhi wengine 113,274. Maelfu zaidi pia wametoweka na inaaminika wamekufa chini ya vifusi.
Mnamo Novemba 21 mwaka jana, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ilitoa hati za kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na waziri wa zamani wa vita Yoav Gallant kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu katika Ukanda wa Gaza.
Israeli pia inakabiliwa na kesi ya mauaji ya kimbari katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kutokana na vita vyake vya kikatili dhidi ya Gaza.