Iran yasisitizia kuharakishwa utekelezaji wa makubaliano kati yake na Qatar
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i124608-iran_yasisitizia_kuharakishwa_utekelezaji_wa_makubaliano_kati_yake_na_qatar
Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amefanya mazungumzo ya simu na Amir wa Qatar na kutilia mkazo wajibu wa kuharakishwa utekelezaji wa makubaliano kati ya nchi hizo mbili na kuimarishwa uhusiano wa kirafiki na ujirani mwema.
(last modified 2025-04-01T02:47:48+00:00 )
Apr 01, 2025 02:47 UTC
  • Iran yasisitizia kuharakishwa utekelezaji wa makubaliano kati yake na Qatar

Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amefanya mazungumzo ya simu na Amir wa Qatar na kutilia mkazo wajibu wa kuharakishwa utekelezaji wa makubaliano kati ya nchi hizo mbili na kuimarishwa uhusiano wa kirafiki na ujirani mwema.

Katika mazungumzo ya simu na Amir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Aal Thani ya Jumatatu jioni, Rais Pezeshkian amempongeza Sheikh Tamim, serikali na taifa la Qatar kwa mnasaba wa maadhimisho ya Sikukuu ya Idul Fitr na kuhimiza kuimarishwa udugu na mshikamano kati ya mataifa ya Kiislamu.

Aidha Rais Pezeshkian ameelezea kufurahishwa na fursa ya mazungumzo hayo ya simu na akasema ana matumaini kwamba watakutana ana kwa ana haraka iwezekanavyo na Amir wa Qatar ili kujadili njia za kuharakisha utekelezaji wa makubaliano kati ya nchi hizi mbili na kuimarisha uhusiano wa kirafiki na kiudugu kati yao.

Katika mazungumzo hayo ya simu, Amir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Aal Thani, ametoa mkono wa salamu za Idul Fitr kwa serikali na wananchi wa Iran na kusema: "Namuomba Mwenyezi Mungu atupe taufiki Yake ili kwa baraka za Sikukuu hii, tuweze kuimarisha zaidi uhusiano adhimu na maalumu kati ya nchi zetu mbili jirani na nchi nyingine za Kiislamu kwa kupitia kuimarisha ushirikiano, umoja na mshikamano kati yetu."

Amir wa Qatar aidha amemkhutubu Rais Pezeshkian akimwambia: "Pia ninatazamia kupata fursa ya kukutana ana kwa ana na wewe Mheshimiwa ili tuweze kujadili masuala yenye maslahi kwa pande zote mbili na kuharakisha utekelezaji wa makubaliano kati yetu."