Mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Yemen, je, Marekani itaweza kufungua njia za Bahari Nyekundu?
Wiki hii, Jeshi la Yemen lilitangaza kuhusika na mfululizo wa mashambulizi yaliyofanyika kwa ustadi wa hali ya juu na kuzitwanga meli za kivita za Marekani, ikiwa ni pamoja na mwanuwari ya USS Harry S. Truman ya Marekani ya kubebea ndege, katika Bahari Nyekundu.
Opereshenei hizo za kishujaa za vikosi vya ulinzi vya Yemen zimefanywa kwa nia ya kuendelea kukabiliana na uvamizi wa Marekani dhidi ya Yemen na kuliunga mkono taifa madhlumu la Palestina.
Msemaji wa Jeshi la Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree amesema wiki hii kuwa, vikosi vya jeshi la nchi hiyo vimefanya operesheni tatu kubwa za kijeshi za kuzitwanga meli za Marekani katika kipindi cha saa 24 zilizopita yaani saa 24 hadi wakati alipokuwa anatangaza habari hiyo. Jenerali Saree alibainisha kuwa, operesheni za kulipiza kisasi zilizofanywa dhidi ya manuwari na meli za kivita za Marekani kwenye Bahari ya Sham zilihusisha kikosi cha makombora, kitengo cha ndege zisizo na rubani cha jeshi la anga pamoja na kikosi cha wanamaji cha jeshi la Yemen. Operesheni hizo ziliendeshwa kwa kutumia makombora mengi ya kivita yaliyotengenezwa nchini Yemen pamoja na kundi la droni.

Operesheni hizo za kishujaa za vikosi vya ulinzi vya Yemen zinaendelea dhidi ya meli za kijeshi za madola vamizi yakiongozwa na Marekani katika Bahari Nyekundu katika hali ambayo Marekani inaendelea kufanya mashambulizi ya kiwendawazimu na kijinai kwenye maeneo ya raia huko Yemen.
Katika taarifa yake, Brigedia Jenerali Yahya Saree alisisitiza kuwa, vikosi vya ulinzi vya Yemen vitaendelea kukuza uwezo wake wa kiulinzi na vitakabiliana vilivyo na jinai zote zinazoongezeka kila kukicha za adui hasa Marekani. Alisisitiza kwamba majeshi ya Yemen hayatarudi nyuma katika kuwaunga mkono watu wanaodhulumiwa wa Palestina hadi mashambulizi ya umwagaji damu yanayoendelea kufanywa na Israel dhidi ya Ghaza yatakapokoma, na mzingiro wa eneo hilo utakapoondolewa kabisa.
Ikumbukwe kuwa lengo la Marekani la kuanzisha wimbi jipya la jinai zake dhidi ya Yemen ni kujaribu kufungua njia za Bahari Nyekundu ili meli na vyombo vya baharini vya Israel na vinavyopeleka bidhaa kwa utawala wa Kizayuni viweze kutumia njia hiyo muhimu mno ya baharini. Lakini wachambuzi wa mambo wanasema, Marekani kamwe haitoweza kufikia malengo yake hayo haramu na kwamba njia pekee ya kuweza kutatua mgogoro huo ni kukomeshwa vita, mzingiro wa Ghaza na jinai za Wazayuni.
Miongoni mwa waliotoa maoni yao kuhusu mashambulizi ya kiuadui ya Marekani dhidi ya Yemen, ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Takht Ravanchi ambaye amesema kuwa, hakuna suluhisho la kijeshi la mgogoro wa Yemen. Amepongeza ushujaa wa vikosi vya ulinzi vya Yemen katika safu zao zote, akisema vinatekeleza majukumu yao ya kidini, kibinadamu na maadili katika kulinda Yemen huru na kuunga mkono Wapalestina wanaodhulumiwa.
Mbali na kuzuia vyombo vya majini kutumia Bahari ya Sham kuelekea Israel, vikosi vya ulinzi vya Yemen vinafanya mashambulizi pia dhidi ya maeneo mbalimbali ya Israel na kuuweka utawala wa Kizayuni katika mazingira na wakati mgumu sana.

Weledi wa mambo wanasema kuwa, miongoni mwa mambo yaliyochangia sana kulazimika Israel kukubali kusimamisha vita baada ya zaidi yamiezi 15 ya jinai zake huko Ghaza, yalikuwa ni mashambulizi ya mara kwa maara ya Jeshi la Yemen kwa maeneo tofauti ya Palestina yaliyopachikwa jina bandia la Israel sambamba na jeshi hilo la Yemen kufunga njia zote za Bahari Nyekundu kwa vyombo vilivyokuwa vinaeleka kwa utawala wa Kizayuni wa Israel. Wataalamu wa masuala ya kiuchumi wanasema kwamba, Israel ilipata hasara kubwa za kiuchumi wakati wa jinai zake za zaidi ya miezi 15 huko Ghaza.
Muqawama wa wananchi Waislamu wa Yemen bila ya shaka yoyote una nafasi kubwa katika kushindwa njama za Marekani na Wazayuni za kujaribu kulipigisha magoti taifa hilo la Kiislamu na Kiarabu. Ushahidi wa Muqawama huo thabiti wa taifa la Yemen umeonekana wakati wa maadhimisho ya sikukuu ya Idul Fitr na kabla ya hapo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds ambapo wananchi wa Yemen walijitokeza kwa mamilioni kutangaza utiifu kwa viongozi wao na uungaji mkono wao usiotetereka kwa taifa madhlumu la Palestina.
Hapana shaka kwamba uungaji mkono mkubwa wa wananchi unazidi kulipa nguvu Jeshi la Yemen kukabiliana kiume na mashambulizi ya kijinai ya Marekani na kama vilivyokiri hata vyombo vya utawala wa Kizayuni wa Israel, kwamba mashambulizi dhidi ya meli za Marekani yataendelea na Washington hawawezi kabisa kuilazimisha Yemen kuruhusu meli za Israel kutumia Bahari Nyekundu.