Israel yampiga marufuku mkurugenzi wa Msikiti wa Ibrahimi kwa siku 15
Utawala haramu wa Israel umempiga marufuku mkurugenzi wa Msikiti wa Ibrahimi ulioko katika mji wa al-Khalil, Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, kuingia katika eneo hilo takatifu la Kiislamu kwa zaidi ya wiki mbili, huku utawala huo ukiendeleza mashambulizi yake ya kikatili dhidi ya Wapalestina na maeneo yao matakatifu.
Shirika la habari la serikali ya Uturuki, Anadolu, liliripoti jana Jumanne kwamba Sheikh Moataz Abu Sneineh amepigwa marufuku kuingia Msikiti wa Ibrahimi kwa muda wa siku 15, baada ya jeshi vamizi la Israel kufunga baadhi ya sehemu za msikiti huo zinazosimamiwa na taasisi ya Kiislamu ya Wakfu.
Jamal Abu Aram, Mkurugenzi wa Idara ya Wakfu ya al-Khalil amesema kuwa marufuku hiyo ni mwendelezo wa mkakati wa Israel wa “kuhodhi msikiti na kuinyang’anya Idara ya Wakfu mamlaka ya kusimamia sehemu zake.”
Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kidini ya Palestina imelaani hatua hiyo na kusema maeneo yote ya msikiti—vikiwemo vyumba vya makaburi na njia zake—ni miliki ya Idara ya Wakfu ya Kiislamu, ambayo ina haki ya kisheria ya kushikilia funguo zake, na imelaani hatua ya kufungwa milango hiyo ikiitaja kuwa ni “shambulio la wazi na la kutisha dhidi ya heshima ya maeneo haya matakatifu.”
Kizuizi hiki kinakuja kufuatia hatua ya utawala wa Israel katika mwezi uliopita wa Ramadhani ya kukataa kufungua sehemu zote za msikiti huo kwa waumini, hata katika matukio muhimu kama vile Idul Fitr, Laylatul-Qadr na Ijumaa, kinyume na ilivyozoleleka.
Tangu mwaka 1994, baada ya mlowezi mmoja wa Kizayuni kuwafaytulia risasi na kuwaua Wapalestina 29 waliokuwa wakiswali katika Msikiti wa Ibrahimi, utawala wa Israel uliugawa msikiti huo, ambapo asilimia 63—kikiwemo chumba cha adhana—ilitengwa kwa ajili ya Wayahudi, huku asilimia 37 ikibaki kwa Waislamu.
Msikiti huo unaendelea kuwa chini ya udhibiti wa Israel, huku takribani wakoloni 400 wa Kiyahudi wakiishi katika Mji Mkongwe wa al-Khalil, wakiwa wanalindwa na askari wa Israel wapatao 1,500.