Wapalestina wengine 40 wauawa shahidi Gaza na mabomu ya Wazayuni
(last modified Thu, 10 Apr 2025 02:54:33 GMT )
Apr 10, 2025 02:54 UTC
  • Wapalestina wengine 40 wauawa shahidi Gaza na mabomu ya Wazayuni

Utawala wa Kizayuni wa Israel umeendelea kumwaga damu za Wapalestina; ambapo umewauwa Wapalestina karibu 40 wakiwemo watoto katika mashambulizi ya anga ya karibuni katika maeneo kadhaa katika Ukanda wa Gaza unaozingirwa.

Jana Jumatano, ndege za kivita za Israel zilishambulia nyumba moja ya makazi katika kitongoji cha Shujaiyya, kilichoko mashariki mwa Jiji la Gaza.

Takriban Wapalestina 30 waliuawa shahidi katika hujuma hiyo. Makumi pia walijeruhiwa katika shambulio hilo dhidi ya jengo la ghorofa kadhaa.

Mamlaka za afya za eneo hilo zimesema Wapalestina wengine tisa wameuawa shahidi katika mashambulizi tofauti ya kijeshi ya Israel katika maeneo mengine ya eneo hilo lililozingirwa la Palestina, na kuongeza idadi ya waliouawa shahidi Jumatano hadi 39.

Ndege za kivita za Israel pia zilishambulia kambi ya wakimbizi ya Nuseirat katikati mwa Gaza. Baadhi ya ripoti za vyombo vya habari zimesema takriban Wapalestina 80 wametoweka.

Jeshi la Israel lilisema jana Jumatano kwamba, ndege zake za kivita zimefanya mashambulizi ya anga katika maeneo 45 katika eneo la Gaza ndani ya saa 24.

Ukatili wa Wazayuni Gaza

Haya yanajiri huku vituo vya afya huko Gaza vikiwa katika hali mbaya. Wizara ya Afya ya Gaza imesema kuwa karibu watoto 60,000 wako katika hatari ya kuathirika kiafya kutokana na utapiamlo.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, Wapalestina wapatao 1,500 wameuawa shahidi na wengine 3,434 wamejeruhiwa tangu utawala wa Kizayuni ulipoanzisha tena mashambulio hayo ya kinyama na mauaji ya kimbari dhidi ya eneo hilo mnamo Machi 18.