Saudi Arabia yaanzisha tena mashambulizi dhidi ya Yemen?
Vyanzo vya ndani nchini Yemen vimeripoti habari ya kujiri mashambulizi ya mizinga na makombora ya Saudi Arabia dhidi ya nchi hiyo jirani yake.
Vyombo vya habari nchini Yemen vimenukuu duru za kiusalama zikisema kuwa, mashambulio hayo ya makombora na mizinga ya Saudia yamelenga maeneo kadhaa ya mkoa wa Sa'ada, kaskazini magharibi ya Yemen.
Hakukuwa na maelezo ya kina kuhusu athari za mashambulizi hayo. Hata hivyo baadhi ya duru za habari zimeeleza kuwa, mashambulizi hayo yamesababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu katika eneo hilo.
Hakuna taarifa iliyotolewa kuhusu idadi ya wahanga na majeruhi wa mashambulizi hayo mapya ya Saudia, ambayo yalikuwa yamesita kwa miaka kadhaa.
Haya yananiri huku Marekani ikiongoza majeshi vamizi ya Magharibi kufanya mashambulizi makali ya anga dhidi ya nchi hiyo maskini ya Kiarabu. Maelfu ya raia, wengi wao wakiwa watoto na wanawake, wameuawa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi kutokana na mashambulizi ya Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya Yemen.
Serikali ya Sana’a imeitaka jamii ya kimataifa kuziwajibisha Tel Aviv, Washington na washirika wao kwa vitendo vyao hivyo vya uchokozi, huku ikionya kuwa, mashambulizi yanayoendelea kufanya yanaweza kuwa na athari mbaya kwa pande zote zinazohusika.
Jeshi la Yemen hata hovyo limesisitiza kuhusu azma yake ya kusimama na kuwapa himaya wananchi wa Palestina na Lebanon, bila kujali mashambulizi na uchokozi wa Israel na Marekani.