Jasusi mzoa taka anaswa kwenye mtego wa vikosi vya Muqawama Ghaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i125280-jasusi_mzoa_taka_anaswa_kwenye_mtego_wa_vikosi_vya_muqawama_ghaza
Vikosi vya Muqawama huko Ghaza vimemnasa kwenye mtego, jasusi wa utawala katili wa Kizayuni wa Israel ambaye alijifanya ni mzoa taka kumbe alikuwa anafanya ujasusi wa kujua walipo mateka wa Kizayuni.
(last modified 2025-04-17T02:12:58+00:00 )
Apr 17, 2025 02:12 UTC
  • Jasusi mzoa taka anaswa kwenye mtego wa vikosi vya Muqawama Ghaza

Vikosi vya Muqawama huko Ghaza vimemnasa kwenye mtego, jasusi wa utawala katili wa Kizayuni wa Israel ambaye alijifanya ni mzoa taka kumbe alikuwa anafanya ujasusi wa kujua walipo mateka wa Kizayuni.

Shirika la Habari la Fars limenukuu taarifa iliyotolewa na afisa mmoja katika kitengo cha usalama cha makundi ya Muqawama ya Palestina akitangaza habari hiyo jana Jumatano na kuongeza kuwa, magenge ya kijasusi ya Israel yalimpa kazi jasusi huyo ya kutafuta na kuripoti ishara zozote zinazohusiana na mateka wa Kizayuni huko Ghaza.

Kwa mujibu wa maelezo ambayo jarida la Al-Harith lililoruhusiwa kuchapisha taarifa hiyo, jasusi huyo mwenye umri wa miaka 33, aliyetajwa kwenye ripoti hiyo kwa jina la kupanga la "T.T," alikamatwa miezi michache iliyopita alipokuwa akifanya ujasusi kupitia kujifanya ni mzoa taka katika Ukanda wa Ghaza.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, jasusi huyo Mzayuni alijiunga na magenge ya kijasusi ya Israeli mwaka 2022 baada ya kuwa na uhusiano na afisa mmoja wa kike wa mashirika ya kijasusi ya Israel.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, afisa huyo wa kike, aliyejifanya mkurugenzi wa shirika la habari za kigeni, alidai anapenda kukusanya simulizi na uzoefu wa wapinzani wa Muqawama katika Ukanda wa Ghaza, na kwa njia hiyo alianza uhusiano wake na jasusi huyo na baadaye kumtumia kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni huko Ghaza.

Jasusi huyo amekiri kwamba alipokea fedha nyingi kutoka nchi mbalimbali kwa kueneza simulizi za uzushi kuhusu jinsi Muqawama ulivyowatendea watu wa Ghaza, pamoja na kufanya uhalifu kama vile wizi, mauaji na ubakaji wa wanawake.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kazi muhimu zaidi iliyofanywa na jasusi huyo ilikuwa ni kutafuta na kuchimba uchafu ili kupata mabaki ya aina mahususi ya chakula ambacho Israel iliruhusu kuingia Ukanda wa Ghaza katika majira ya joto ya mwaka 2024.

Magenge ya kijasusi ya Israel yalimtaka jasusi huyo kutafuta mada hizo kwa kisingizio cha kukusanya "plastiki na mbao" na kuripoti ishara zozote zinazohusiana na waliko mateka wa Kizayuni huko Ghaza.

Kamanda mmoja katika idara ya usalama ya Muqawama amesema: "Tumeweza kunasa taarifa nyingi za ujasusi uliofanywa kwenye Ukanda wa Ghaza wa kujaribu kugundua walipo mateka wa maadui lakini haziwezi kutangazwa hadharani hivi sasa."