Wapalestina 18 wauawa shahidi katika unyama mwingine wa Israel
Mashambulizi ya leo ya utawala haramu wa Israel katika maeneo mbalimbali ya Gaza yamesababisha vifo vya watu 18 na wengi kujeruhiwa.
Ripoti zinasema kuwa, katika mashambulio ya leo ya ndege za kivita za Israel kwenye mkusanyiko wa raia kwenye mtaa wa Al-Nakheel katika kitongoji cha Al-Sha'af, watu 5 waliuawa shahidi, na miili yao kuhamishiwa katika hospitali ya Al-Ma'madani.
Kwa mujibu wa ripoti hii, maeneo mbalimbali, likiwemo eneo la Al-Qarn, mashariki mwa Jabalia, na Beit Hanoun, pia yalilengwa na mashambulizi ya mizinga ya Israel hii leo, na helikopta pia zilifyatulia baadhi ya maeneo.
Kwa mujibu wa ripota wa Al-Alam, maeneo ya kusini mwa Ukanda wa Gaza yalilengwa na ndege za kivita za Israel, na watu watano waliuawa shahidi katika shambulio lililolenga kituo cha mikusanyiko ya raia katika eneo la Safa.
Pia, watu wawili waliuawa shahidi katika shambulio katika eneo la kati la Ukanda wa Gaza mapema asubuhi ya leo, ambalo lililenga nyumba ya familia ya Darwish katika eneo la kambi ya wakimbizi ya Nuseirat.
Wakati huo huo, Wizara ya Afya ya Palestina imetahadharisha kuwa, watu 200,000 wenye maradhi thakili wako hatarini kupoteza maisha kutokana na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel kuendelea kuvifunga vivuko, jambo ambalo linavuruga pia utendaji kazi wa hospitali katika Ukanda huo.