Qatar yalaani mpango wa Wazayuni wa kubomoa Msikiti wa Al-Aqswa
Qatar imelaani vikali mpango wa taasisi za Wazayuni wenye misimamo mikali ya kubomoa msikiti wa Al-Aqswa katika mji wa Baytul-Muqaddas.
Qatar imetoa mwito wa kuchukuliwa hatua za haraka na jamii ya kimataifa kuilazimisha Tel Aviv kuheshimu maeneo matakatifu ya Waislamu.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo imeuona wito wa taasisi za utawala ghasibu kwa mabavu kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii wa kuushambulia kwa mabomu na kuuharibu msikiti wa Al-Aqsa na kujenga hekalu kuwa ni mpango hatari na kuongeza kuwa, mpango huo katika kivuli cha vita vya hivi sasa dhidi ya Ukanda wa Gaza, utapelekea kushadidi machafuko katika eneo hili.
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Qatar sambamba na kulaani vikali ukiukaji wowote wa hadhi ya kihistoria na kisheria ya msikiti wa Al-Aqswa, Baytul-Muqaddas na maeneo yake matakatifu, imesisitiza ulazima wa kuchukuliwa hatua za haraka na jamii ya kimataifa ili kuzuia uvamizi huo, kuulazimisha utawala wa Kizayuni kutoa ulinzi unaohitajika kwa maeneo hayo matakatifu, na kuheshimu maazimio ya uhalali wa kimataifa.
Katika miezi ya hivi karibuni vitendo vya hujuma na uvamizi wa walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina hususan katika Msikiti wa al-Aqswa vimeongezeka mno.
Utawala wa Kizayuni ambao unaungwa mkono kikamilifu na Marekani katika hatua zake hizo haramu umedhamiria kubadilisha muundo wa kijiografia na kidemografia wa maeneo ya Palestina; ili kuyazayunisha maeneo hayo na kuhakikisha unazihodhi na kuzidhibiti kikamilifu ardhi za Wapalestina.