Jinamizi la kukwama safari za ndege laendelea kuitesa Israel
Mashambulizi ya Jeshi la Yemen dhidi ya viwanja vya ndege vya utawala wa Kizayuni hususan Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion wa Tel Aviv yanaendelea kuisababishia jinamizi Israel hususan baada ya Yemen kuapa kuvigeuza Jahannam viwanja hivyo vya utawala wa Kizayuni mpaka ukomeshe jinai zake huko Ghaza.
Wimbi la kusimamishwa safari za ndege za kutoka na kuingia Israel limewaacha maelfu ya abiria katika nchi mbalimbali duniani kuemewa na hawajui cha kufanya.
Kwa mujibu wa Pars Today, mashirika ya ndege kutoka nchi kadhaa zikiwemo za Ulaya kama Ujerumani, Uswizi, Uhispania na Italia pamoja na nchi za Asia kama India, yameendelea kurefusha muda wa kufuta safari zao za ndege kuelekea Tel Aviv yakisema kuwa hali si salama huko Israel.
Msemaji wa shirika la ndege la Ujerumani la Lufthansa ametangaza kuwa, kundi la Lufthansa linalojuisha pamoja mashirika kadhaa ya ndege limesimamisha safari zake zote za kuelekea Israel kwa muda usiojulikana na hadi tangazo jingine litakapotolewa.
Mashirika mengine kama ya Swiss Air na Air India nayo yamechukua uamuzi huo huo. Duru rasmi za mashirika hayo zimesisitiza kwamba usalama wa abiria na wafanyakazi wa ndege ndicho kipaumbele cha kwanza na kwamba yatarejesha safari zao kuelekea Israel kama hali ya usalama itarejea. Shirika la ndege la Italia ITA pia lilitangaza jana Jumamosi kwamba limerefusha uamuzi wake wa kufuta safari zake zote za ndege kuelekea Israel hadi Mei 19.
Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa kuendelea jinamizi hilo kwa Israel kuna athari kubwa za kiuchumi na kisiasa kwa utawala wa Kizayuni na hasa kwa serikali ya kifashisti ya Benjamin Netanyahu inayofanya jinai za kutisha dhidi ya Wapalestina hasa wa Ghaza.