Israel yafanya mauaji mengine ya kutisha Gaza, yaua zaidi ya 103 leo Alkhamisi
(last modified Thu, 15 May 2025 11:41:58 GMT )
May 15, 2025 11:41 UTC
  • Israel yafanya mauaji mengine ya kutisha Gaza, yaua zaidi ya 103 leo Alkhamisi

Idadi ya Wapalestina waliouawa katika mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza tangu alfajiri ya Alhamisi ya leo mepindukia 103. Utawala vamizi wa Israel umezidisha mashambulizi yake ya anga dhidi ya watu wa Gaza, sanjari na ziara ya sasa Rais wa Marekani, Donald Trump, Mashariki ya Kati iliyoanza Jumanne iliyopita.

Televisheni ya Al Jazeera ya Qatar imenukuu vyanzo vya matibabu vya Palestina, kwamba takriban watu 60, wakiwemo wanawake na watoto, wameuawa katika shambulio la Israel huko Khan Yunis kusini mwa Ukanda wa Gaza pekee.

Ripoti zinasema kuwa, mashahidi na majeruhi wamehamishiwa katika eneo la Nasser Medical Complex lililokuwa limejaa majeruhi na miili ya mashahidi, huku uhaba mkubwa wa vifaa vya matibabu ukiendela kushuhudiwa katika hospitali za Ukanda wa Gaza.

Mashambulizi na mauaji ya jeshi la Israel yameendelea kushuhudiwa tangu mapema leo alfajiri katika maeneo mbalimbali ya Ukanda wa Gaza na hadi tunaandika habari hii idadi ya Wapalestina waliouawa ilikuwa imepindukia 103. 

Harakati ya mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imelaani mauaji ya Israel katika Ukanda wa Gaza na kusema kuwa, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amezidisha kasi ya mauaji dhidi ya raia wasio na hatia ili kudhoofisha juhudi zinazofanywa hivi sasa na wapatanishi kwa ajili ya kusitisha vita na kukamilisha makubaliano ya kubadilishana mateka na wahabusu.