Ansarullah: Iran imetekeleza wajibu wake wa Kiislamu kuiunga mkono Palestina
Kiongozi wa Harakati ya Muqawama ya Ansarullah ya Yemen ameipongeza Iran kwa uungaji mkono wake usio na kikomo kwa taifa la Palestina na kadhia yao halali na kueleza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inafuata njia ya heshima katika suala hilo na nchi nyingine zote za Kiislamu lazima zifuate mkondo huo.
Abdul-Malik al-Houthi alisema hayo katika hotuba yake kwa njia ya televisheni kutoka mji mkuu wa Yemen Sana'a jana Alkhamisi na kuongeza kuwa, "Iran inafuata mbinu ya Kiislamu ya kupongezwa kwa kukumbatia malengo ya Palestina na kuwaunga mkono wapiganaji wa Muqawama. Hiki ndicho kila taifa la Kiislamu linapaswa kufanya."
Amebainisha kuwa, "Msimamo wa Iran ni wa Kiislamu unaopasa kupongezwa kwa kuwa unalenga kuunga mkono kadhia ya Palestina. Jamhuri ya Kiislamu imethibitisha na kutekeleza wajibu wake wa Kiislamu kwa kuisaidia Palestina."
Kiongozi huyo wa Ansarullah ya Yemen aidha amezikosoa nchi za Kiarabu kwa kushindwa kwao kuchukua misimamo madhubuti kuhusiana na kadhia ya Palestina na kusema kwamba, mbinu zao rasmi zimeshindwa kuunda njia ya kivitendo na iliyo wazi ya kuunga mkono kikweli kadhia hiyo tukufu.
Amesema kukosekana kwa umoja wa Waarabu kumeathiri kadhia ya Palestina katika ngazi ya kimataifa, ambapo tawala za Kiarabu zinapendekeza tu mafundisho ya kufedhehesha ya kusalimu amri na kuridhiana.
Al-Houthi amesisitiza haja ya kuangaliwa upya kwa kina sera na misimamo ya ulimwengu wa Kiislamu ili kukabiliana na uvamizi wa Wazayuni na kuliunga mkono taifa la Palestina.