Jinai za Israel ni kubwa mpaka UK, Canada na Ufaransa zatishia kuiwekea vikwazo
Jinai za utawala wa Kizayuni ni kubwa mno na hazivumiliki kiasi kwamba hata viongozi wa Uingereza, Canada na Ufaransa wametishia kuiwekea vikwazo Israel kutokana na uhalifu wa kivita na jinai za kutisha huko Ghaza. Tishio hilo limezidisha mashinikizo kwa nduli wa Ghaza, yaani waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.
Ingawa tishio hilo lililotolewa na Uingereza, Canada na Ufaransa limetolewa kwa kuchelewa sana, lakini ni uthibitisho mwingine kwamba jeshi la Israel chini ya Benjamin Netanyahu linafanya ukatili na jinai kubwa kupindukia kiasi kwamba hata waitifaki wa karibuni mno wa utawala wa Kizayuni hawawezi tena kuvumilia.
"Kitendo cha serikali ya Israel cha kuwanyima raia msaada muhimu wa kibinadamu hakikubaliki na kuna hatari ikwa ni kukanyaga Sheria ya Kimataifa ya Kibinadamu," imesema taarifa ya pamoja ya nchi hizo tatu za Magharibi, iliyotolewa na serikali ya Uingereza.
Sehemu nyingine ya taaria hiyo imesema: "Tunapinga jaribio lolote la kupanua makazi katika Ukingo wa Magharibi... Hatutasita kuchukua hatua zaidi, ikiwa ni pamoja na vikwazo."
Israel imezuia kuingia vifaa vya matibabu, chakula na mafuta Ghaza tangu mwanzoni mwa mwezi Machi mwaka huu wakati ilipoanzisha wimbi jipya la jinai zake na baada ya kukanyaga makubaliano ya kusimamisha vita kati yake na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, HAMAS.
Viongozi wa nchi hizo tatu za Uingereza, Canada na Ufaransa aidha wamesema kuwa wanaunga mkono juhudi za kusitishwa mara moja mashambulizi ya Israel huko Ghaza, na kudai kuwa wamejitolea kulitambua taifa la Palestina kama nchi huru.
Hamas imekaribisha taarifa hiyo ya pamoja ya nchi tatu za Magharibi za Uingereza, Canada na Ufaransa.