HAMAS yakabidhi mapendekezo yake kuhusu makubaliano ya kusitisha vita Ghaza
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imesema katika taarifa iliyotoa mapema leo kwamba "imewasilisha majibu yake na yale ya makundi ya Wapalestina" kwa wapatanishi baada ya majuma kadhaa ya mazungumzo ya kusitisha mapigano yaliyoshindwa kuzaa matunda.
Majibu hayo ya Hamas yanaripotiwa kuwa ni pamoja na marekebisho ya masharti kuhusu uingizwaji wa misaada katika Ukanda wa Ghaza, sehemu za eneo hilo ambazo jeshi la utawala wa kizayuni litapaswa kuondoka, na kupatiwa dhamana na hakikisho la kukomeshwa vita kikamilifu.
Hayo yanajiri huku jeshi la utawala ghasibu wa Israel likiwa linaendelea kulishambulia kwa mabomu na makombora eneo la Ghaza, ambapo kwa jana pekee liliwaua shahidi Wapalestina wasiopungua 77, wakiwemo watu 25 wanaotafuta misaada ya chakula.
Ripoti za hivi punde kutoka Ghaza zinaeleza kuwa, tokea mapambazuko ya leo hadi wakati huu, jeshi la utawala wa kizayuni limeshawaua shahidi Wapalestina 23, wakiwemo tisa wanaohangaika kutafuta msaada wa chakula.
Wakati huohuo, muungano wa mashirika 109 ya misaada umeonya juu ya ulichokiita "mateso ya njaa ya halaiki" yanayowakabili Wapalestina huko Ghaza na kutoa wito wa kusitishwa mara moja mapigano na kuondolewa vizuizi vyote vilivyowekwa dhidi ya ufikishaji wa misaada ya kibinadamu katika eneo hilo la Palestina lililowekewa mzingiro…/