Israel yaua Wapalestina wengine 60, yashadidisha ukatili wake 'Gaza City'
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i129660-israel_yaua_wapalestina_wengine_60_yashadidisha_ukatili_wake_'gaza_city'
Jeshi la Israel limeshadidisha mashambulizi katika Jiji la Gaza kama sehemu ya operesheni zake zilizopanuliwa zenye lengo la kuteka na kukalia kwa mabavu eneo hilo la 'mwisho' lenye idadi kubwa ya watu katika Ukanda wa Gaza, na kulazimisha makumi ya maelfu ya Wapalestina wanaokabiliwa na njaa kukimbia tena.
(last modified 2025-09-22T12:10:58+00:00 )
Aug 18, 2025 06:43 UTC
  • Israel yaua Wapalestina wengine 60, yashadidisha ukatili wake 'Gaza City'

Jeshi la Israel limeshadidisha mashambulizi katika Jiji la Gaza kama sehemu ya operesheni zake zilizopanuliwa zenye lengo la kuteka na kukalia kwa mabavu eneo hilo la 'mwisho' lenye idadi kubwa ya watu katika Ukanda wa Gaza, na kulazimisha makumi ya maelfu ya Wapalestina wanaokabiliwa na njaa kukimbia tena.

Jiji la Gaza lilikuwa mlengwa mkuu wa mashambulizi ya anga ya Israel jana Jumapili ambayo yaliwauwa shahidi karibu watu 60 - ikiwa ni pamoja na watu 37 waliokuwa wakisubiri chakula cha msaada- wakati Israel ikishadidisha mashambulizi dhidi ya mji mkubwa zaidi wa Gaza.

Vitongoji vya Jiji la Gaza vya Zeitoun, Sabra, Remal na Tuffah ndivyo vilivyolengwa zaidi na mashambulizi ya Israel katika siku za hivi karibuni, huku Msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu akisema mipango ya Israel ya kuwahamisha Wapalestina kwa nguvu hadi kusini mwa Gaza haitakuwa na matokeo mengine ghairi ya kuwaongeza mateso Wapalestina hao.

Kwa mujibu wa Al-Jazeera, maelfu ya familia zimeikimbia Zeitoun, ambapo siku kadhaa za hujuma zinazoendelea zimekiacha kitongoji hicho kikiwa kimeharibiwa kikamilifu.

Watu wasiopungua saba waliuawa shahidi jana Jumapili wakati wa mashambulizi ya anga ya Israel yaliyolenga Hospitali ya al-Ahli Arab katika Jiji la Gaza.

Vita vya kikatili vya Israel dhidi ya Gaza vimeua shahidi takriban watu 61,827 na kujeruhi 155,275 tokea Oktoba 7, 2023, hadi sasa.