Jeshi la Yemen lashambulia maeneo nyeti ya Israel kwa kombora la kasi ya juu la “Palestine-2”
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i130752-jeshi_la_yemen_lashambulia_maeneo_nyeti_ya_israel_kwa_kombora_la_kasi_ya_juu_la_palestine_2
Jeshi la Yemen limetangaza kuwa limevurumisha kombora la kasi ya juu au haipasoniki aina ya “Palestine-2” lenye vichwa vingi vya mlipuko dhidi ya maeneo nyeti ndani ya Tel Aviv, katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu yaani 'Israel'.
(last modified 2025-09-13T08:11:35+00:00 )
Sep 13, 2025 08:11 UTC
  • Jeshi la Yemen lashambulia maeneo nyeti ya Israel kwa kombora la kasi ya juu la “Palestine-2”

Jeshi la Yemen limetangaza kuwa limevurumisha kombora la kasi ya juu au haipasoniki aina ya “Palestine-2” lenye vichwa vingi vya mlipuko dhidi ya maeneo nyeti ndani ya Tel Aviv, katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu yaani 'Israel'.

Katika taarifa iliyotolewa Jumamosi, Jeshi la Yemen limebaini kuwa operesheni hiyo ni jibu kwa “uhalifu wa mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Gaza,” pamoja na “uchokozi wa utawala wa Kizayuni dhidi ya Yemen.”

Taarifa hiyo imesema kuwa operesheni hiyo “imefanikiwa kwa neema ya Mwenyezi Mungu,” na kusababisha “makundi ya mamilioni ya Wazayuni waporaji kukimbilia mafichoni.”

Jeshi la Yemen limeapa kuendeleza mashambulizi kwa ajili ya kulinda taifa lao na kuunga mkono “ndugu zetu wa Gaza walioko mstari wa mbele, hadi uvamizi dhidi yao usitishwe na mzingiro kuondolewa.”

Mapema Jumamosi, vyombo vya habari vya Israel viliripoti kuwashwa kwa ving’ora vya tahadhari katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu kufuatia kombora lililokuwa likielekezwa Tel Aviv na miji mingine.

Tukio hilo limejiri siku mbili baada ya Jeshi la Yemen kudai kuhusika na mashambulizi ya anga dhidi ya maeneo ya Israel kwa kutumia kombora la kasi ya juu na ndege tatu zisizo na rubani. Msemaji wa jeshi hilo, Brigedia Jenerali Yahya Saree, alisema Alhamisi kuwa kombora na droni moja vililenga maeneo maalumu katika jangwa la Negev, huku droni nyingine mbili zikielekezwa Uwanja wa Ndege wa Ramon katika mji wa Eilat kusini mwa 'Israel'. Alieleza mashambulizi hayo kama “yaliyofanikiwa.”

Kutokana na vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendelezwa na Israel Gaza tangu Oktoba 2023, Yemen imekuwa ikitekeleza mzingiro wa kimkakati wa baharini kwa lengo la kuzuia usafirishaji wa silaha kwenda Israel, huku ikitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua kuhusu janga la kibinadamu linaloendelea Gaza.

Jeshi la Yemen pia linaendeleza mashambulizi kadhaa ya makombora na droni dhidi ya maeneo muhimu ndani ya utawala wa Israel kwa lengo la kubainisha mshikamano wake na Wapalestina wa Gaza.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, Israel imewaua Wapalestina wasiopungua 64,756—wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto—tangu Oktoba 2023.