Hizbullah: Mpango wa Trump wa Gaza unalenga 'kuisafisha' Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i131640-hizbullah_mpango_wa_trump_wa_gaza_unalenga_'kuisafisha'_israel
Katibu Mkuu wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon, Sheikh Naim Qassem amekosoa mpango wa Rais wa Marekani, Donald Trump kuhusu Gaza, na kuutaja kuwa ni hatua hatari ya kuisafisha Israel kutokana na jinai zake na sehemu ya ajenda ya kujitanua utawala huo ghasibu.
(last modified 2025-10-06T02:37:40+00:00 )
Oct 06, 2025 02:37 UTC
  • Hizbullah: Mpango wa Trump wa Gaza unalenga 'kuisafisha' Israel

Katibu Mkuu wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon, Sheikh Naim Qassem amekosoa mpango wa Rais wa Marekani, Donald Trump kuhusu Gaza, na kuutaja kuwa ni hatua hatari ya kuisafisha Israel kutokana na jinai zake na sehemu ya ajenda ya kujitanua utawala huo ghasibu.

Akihutubia hafla ya kuadhimisha kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kuuawa shahidi makamanda wawili wakuu wa Hizbullah, Sheikh Nabil Qawouk na Sayyid Suhail Al-Husseini, Sheikh Qassem alionya kwamba, Marekani inausaidia utawala wa Tel Aviv katika kutimiza ndoto yake ya kile kinachoitwa "Israel Kubwa Zaidi."

"Kinachotokea Gaza leo ni sehemu ya mpango wa 'Israel Kubwa Zaidi' ambao unafuatiliwa kwa uungaji mkono kamili wa Marekani," amesema akirejelea mpango wa Trump wa kusitisha mapigano Gaza wenye nukta 20, ambao wakosoaji wanasema umepuuza hali halisi ya Wapalestina.

Katibu Mkuu wa Hizbullah amesisitiza kuwa, "mpango wa Trump unaendana kabisa na maslahi ya Israel. Ni mradi ambao wanataka kupasisha kupitia siasa, kwa kuwa walicshindwa kufikia kupitia uchokozi na uhalifu."

Sheikh Qassem ameongeza kuwa, "Kuiondoa Israel katikati ya ghadhabu iliyoenea duniani, hasa kupitia Umoja wa Mataifa, pamoja na misimamo ya watu wengi Marekani na nchi za Ulaya, ni sehemu nyingine ya mpango wa kupamba sura ya utawala huo,"

Mwanachuoni huyo wa Kiislamu nchini Lebanon ameongeza kuwa, msafara wa kimataifa wa Sumud kutoka makumi ya nchi duniani kwenda kuvunja mzingiro wa Gaza umeonyesha kiwango cha kuporomoka kwa Israel kimataifa kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa.