UN yaitaka Bahrain ikomeshe ukandamizaji dhidi ya Mashia
Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wameutaka utawala wa Aal-Khalifa wa Bahrain uache kuwakandamiza Waislamu wa madhehebu ya Shia na kusisitiza kuwa dhulma hizo ni ukiukaji wa haki za msingi za binadamu.
Taarifa iliyotolewa leo Jumanne na wataalamu huru wa Umoja wa Mataifa imewataka watawala wa Bahrain kukomesha kamatakamata zao dhidi ya Mashia sanjari na kuwaachia huru wale wote waliokamatwa kwa kushiriki maandamano ya amani, ambayo ni haki yao ya msingi.
Kadhalika taarifa hiyo ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa imevitaka vikosi vya usalama vya utawala wa Manama kuondoa vikwazo vya kutembea vilivyowawekea Waislamu wa madhehebu ya Shia na watetezi wa haki za binadamu nchini humo. Aidha wataalamu wa UN wameeleza wasi wasi wao kutokana na wimbi la kuwavua uraia shakhsia wa kidini wanaoipinga serikali ya nchi hiyo ya Ghuba ya Uajemi.
Hii ni katika hali ambayo, wahadhiri wa Chuo Kikuu cha al Azhar nchini Misri wametangaza kuwa, mazungumzo ya kiadilifu yanahitajika nchini Bahrain kwa ajili ya kuheshimu matakwa ya wananchi na kukomesha mgogoro wa sasa nchini humo. Wanazuoni wa Chuo Kikuu cha al Azhar nchini Misri wamesema kuwa, kuzuiwa Swala kubwa zaidi ya Ijumaa ya Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Bahrain ni hatua hatari inayowalenga Mashia nchini humo.
Tangu mwezi Februari mwaka 2011, Bahrain imekuwa uwanja wa maandamano ya amani ya kupinga utawala wa kifalme wa ukoo wa Aal-Khalifa, kushinikiza uhuru na kutekelezwa uadilifu, kuondolewa ubaguzi na kuweko madarakani utawala uliochaguliwa na wananchi wenyewe. Hata hivyo utawala wa Aal Khalifa umekuwa ukijibu matakwa ya wananchi hao kwa mkono wa chuma na ukandamizaji mkubwa.