Wapalestina 14, wakiwemo watoto, wafariki dunia Gaza kutokana na baridi kali
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i134246-wapalestina_14_wakiwemo_watoto_wafariki_dunia_gaza_kutokana_na_baridi_kali
Wapalestina wasiopungua 14 wamepoteza maisha na wengine kadhaa wamejeruhiwa katika kipindi cha chini ya saa 24 huku baridi na dhoruba kali ikiendelea kunguruma katika Ukanda wa Gaza, na kuangusha majengo na miundo mbinu katika maeneo kadhaa.
(last modified 2025-12-13T11:00:36+00:00 )
Dec 13, 2025 06:58 UTC
  • Gaza
    Gaza

Wapalestina wasiopungua 14 wamepoteza maisha na wengine kadhaa wamejeruhiwa katika kipindi cha chini ya saa 24 huku baridi na dhoruba kali ikiendelea kunguruma katika Ukanda wa Gaza, na kuangusha majengo na miundo mbinu katika maeneo kadhaa.

Vyanzo katika hospitali za Gaza vimesema kwamba "watu 14 - wakiwemo watoto 6 - wamefariki dunia kutokana na baridi na zaidi ya nyumba 15 zimeanguka katika maeneo kadhaa ya Jiji la Gaza," huku watu waliokimbia makazi yao wanaoishi katika mahema yaliyochakaa, wakijitahidi kuwalinda watoto wao kutokana na baridi kali, bila rasilimali au uwezo wowote.

Wakati huo huo, wafanyakazi wa ambulensi na Ulinzi wa Raia wameopoa miili ya Wapalestina wanne, wakiwemo watoto wawili, baada ya nyumba kuanguka katika eneo la Bir al-Na’ja, kaskazini mwa Ukanda wa Gaza.

Timu za uokoaji zinaendelea kushughulikia matukeo ya kuanguka nyumba na kutafuta manusura katika hali ngumu ya hewa.

Kwa upande wake, Farhan Haq, Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, amesema kwamba zaidi ya watu 140,000 wameathiriwa na mvua kubwa iliyosababisha mafuriko katika maeneo zaidi ya 200 ya wakimbizi katika Ukanda wa Gaza.

Farhan Haq amesisitiza udharura wa kuondoa vikwazo vya kuingizwa misaada katika ukanda huo, akitilia mkazo ulazima la kuondoa marufuku ya kazi ya Shirika la Misaada na Kazi la Umoja wa Mataifa kwa Wakimbizi wa Palestina (UNRWA).