Onyo la Wapalestina kwa utawala ghasibu wa Israel
Kushadidi uvamizi na hujuma za utawala wa Kizayuni wa Israel katika eneo la Ukanda wa Gaza katika siku za hivi karibuni, kumekabiliwa na radiamali mbalimbali za Wapalestina.
Kuhusiana na hilo, Mushir al-Masri, msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kuwa, mashambulio mapya ya anga ya Israel dhidi ya Gaza kwa mara nyingine tena yameonyesha kuwa, utawala huo katu si wenye kuheshimu usitishaji vita.
Mushir al-Masri amebainisha kwamba, mapambano na muqawama wa Palestina unatoa onyo kwa Israel dhidi ya kuendelea mashambulio yake na unatangaza kuwa, kila uchokozi utakabiliwa na jibu na radiamali kali. Makundi ya mapambano ya Palestina yametangaza kuwa, hayatayanyamazia kimya mashambulio ya Israel pamoja na ukiukaji wake wa usishaji vita na kwamba, yatajibu chokochoko hizo kwa nguvu zote.
Makubaliano ya usitishaji vita baina ya muqawama wa Palestina na utawala haramu wa Israel yalitiwa saini Agosti mwaka 2014 kwa usimamizi wa Misri baada ya mashambulio ya siku 50 ya jeshi la utawala huo dhidi ya Ukanda wa Gaza. Mashambulio ya wanajeshi wa Israel kwa wakazi wa Gaza yanaendelea katika hali ambayo, utawala huo ghasibu kuanzia mwaka 2007 ulishadidisha mzingiro dhidi ya eneo hilo na kuzuia kuingizwa huko bidhaa muhimu na za kimsingi kama mafuta, dawa na vifaa vya ujenzi.
Vitisho na hatua za kupenda vita za Israel ambazo zilidhihirika zaidi baada ya kufunuliwa pazia la madai ya kupenda amani zinatokana na kushindwa mazungumzo eti ya mapatano. Kimsingi hatua hizo za Israel zimezidi kudhihirisha sura halisi ya utawala huo ghasibu.
Kuendelea mzingiro dhidi ya Gaza na hujuma za mara kwa mara za Israel dhidi ya maeneo ya Wapalestina hususan katika Ukanda wa Gaza kunashuhudiwa baada ya kupita muda mrefu tangu kutangazwa usitishaji vita huko Gaza na utawala huo sio tu kwamba, haujaheshimu ahadi yake yoyote ile katika usitishaji vita huo, likiwemo suala la kutochukua hatua yoyote ya kihasama na ya kiuchochezi dhidi ya Wapalestina, bali umeendeleza siasa zake zilizo dhidi ya Wapalestina wasio na ulinzi.
Israel inaendeleza uvamizi na hujuma zake dhidi ya Gaza katika hali ambayo, katika miaka ya 2008, 2012 na 2014 licha ya kufanya mashambulio makubwa dhidi ya eneo hilo na kuua maefu ya watu wasio na hatia, katu haukufanikiwa kufikia hata moja ya malengo yake.
Miamala hii ya utawala wa Kizayuni wa Israel inabainisha wazi kwamba, hakuna wakati ambao utawala huo ulikuwa ni wenye kufuatilia amani katika Mashariki ya Kati. Hapana shaka kuwa, kugonga mwamba utawala huo kisiasa na kijeshi mbele ya mapambano na muqawama wa wananchi katika Mashariki ya Kati, kivitendo kumeutia kiwewe na wahaka mkubwa.
Ni kutokana na sababu hiyo, ndio maana hivi sasa Israel inashadidisha vitisho na harakati za kijeshi ukijidanganya kwamba, kwa njia hiyo unaweza kufunika aibu ya kushindwa kwake na muqawama wa wananchi.
Ukweli wa mambo ni kuwa, Israel imekuwa tayari kutumia fursa yoyote ile kwa ajili ya kusukuma mbele gurudumu la siasa zake za kupenda kujitanua na pale unapoona kuwa una uwezo wa kuanzisha vita basi huwa hausiti hata kidogo kufanya hivyo.
Vita vingi vilivyoanzishwa na utawala huo dhidi ya wananchi wa Palestina na wa mataifa mengi katika Mashariki ya Kati tangu kuasisiwa kwake ni ushahidi tosha wa kuthibitisha hilo.
Jambo lililowazi ni kuwa, miamala ya Israel haijasimama juu ya misingi ya akili na mantiki na viongozi wa utawala huo wamekumbwa na hali ya kuchanganyikiwa iliyosababishwa na kuchezea vipigo kutoka kwa muqawama wa wananchi wa Mashariki ya Kati. Matukio ya miamala ya utawala wa Kizayuni wa Israel yanaonyesha kwamba, yumkini viongozi wa utawala huo wakachukua hatua nyingine ya kijinga.
Ni kwa kuzingatia uhakika huo, ndio maana mataifa ya Mashariki ya Kati likiwemo taifa madhulumu la Palestina daima yamejitayarisha kikamilifu kwa ajili ya kukabiliana na utawala huo ghasibu. Katika mazingira kama haya, kuhifadhi moyo wa muqawama na kuuimarisha ni jambo lenye nafasi muhimu katika kukabiliana na chokochoko yoyote ya Israel pamoja na hatua yoyote ile ya kijinga. Huu ni ukweli ambao umekuwa ukitiliwa mkazo mara kwa mara na makundi ya mapambano ya Palestina.